// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); TUIHURUMIE SIMBA SC, TUSICHOCHEE KUNI - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE TUIHURUMIE SIMBA SC, TUSICHOCHEE KUNI - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Wednesday, March 06, 2013

    TUIHURUMIE SIMBA SC, TUSICHOCHEE KUNI

    Na Bin Zubeiry

    KATIKA siku ya safari, inagundulika Haruna Moshi ‘Boban’ hawezi kusafiri na timu yake, Simba SC kwa ajili ya mchezo wa marudiano, Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika, dhidi ya wenyeji Recreativo de Libolo nchini Angola.
    Timu inawasili Angola, kiungo Mwinyi Kazimoto Mwitula naye anaibua maumivu ya jino, yaliyomfanya ashindwe kufanya mazoezi, hatimaye kushindwa kuanza katika kikosi cha kwanza.
    Wakati huo huo, wachezaji wanne wa kikosi cha kwanza, Paul Ngalema, Jonas Mkude, Edward Christopher na Ramadhani Singano ‘Messi’ hawakusafiri na timu kwa sababu ni majeruhi.
    Hiyo ni timu ambayo ilikuwa ina deni la kukipiku kipigo cha bao 1-0 nyumbani ili kusonga mbele katika michuano hiyo mikubwa Afrika.
    Hakika ulikuwa mtihani mkubwa ambao kama Simba SC ingefuzu, ingestahili pongezi nzito. Simba ilifungwa 4-0 na kutolewa, bao la kwanza ikifungwa ndani ya dakika 10 za mwanzo na matatu mengine, dakika 10 za mwisho.
    Kwa mujibu wa Zacharia Hans Poppe, Mjumbe wa kamati ya Utendaji ya Simba, wachezaji walipambana na hata bao walilofungwa, lilitokana ama na udhaifu wa beki Amir Maftah, au ubora zaidi wa kiungo Dorivaldo Dias.
    Dias alibadilishiwa mtu kipindi cha pili, Kiggi Makassy aliyechukua nafasi ya Maftah, lakini haikuwa dawa ya kutosha.
    Kiungo kinda Abdallah Seseme alipewa jukumu la kupambana na wale viungo hodari wa Libolo tuliowaona Dar es Salaam wakimhenyesha Mwinyi Kazimoto. 
    Ukitazama wachezaji aliobaki nao kocha Mfaransa, Patrick Liewig Angola dhahiri ilikuwa ni pasua kichwa kwake katika kupanga timu. Ramadhan Chombo ‘Redondo’ tumemuona katika mechi za karibuni Uwanja wa Taifa, hayuko katika ubora wake na haikuwa ajabu Salim Kinje kuanzishwa badala yake.
    Liewig alirudia maarifa yale yale ya mechi ya kwanza akilala 1-0 Dar es Salaam, kumuanzishia benchi Mrisho Ngassa ili kipindi cha pili aingie kwenda kubadilisha mchezo kwa kasi yake. Kweli alifanikiwa, lakini hakuwa na madhara zaidi. 
    Nimepitia maoni ya wachambuzi na Waandishi wa Habari baada ya Simba SC kutolewa, wengi wanautupia lawama uongozi na kocha hawafai.
    Kocha anaambiwa anatumia mfumo mbaya, hasa kumpanga Kinje na kumchezesha Kiemba pembeni katika mechi ya marudiano. Badala ya Kinje angempanga nani? Hakuwa na Jonas Mkude, Haruna Moshi, Mwinyi Kazimoto, Ramadhani Singano wala Edward Christopher na Redondo hayuko vizuri.
    Na kama tayari amemchezesha Shomary Kapombe kama kiungo mkabaji na mbele yake Abdallah Seseme, Kiemba angemchezesha wapi? Ni mara ngapi tunamuona Kiemba akishambulia vizuri tu kutokea pembeni tangu enzi za Profesa Milovan Cirkovick?
    Kitu ambacho wanasahau kabla ya kumnyooshea kidole kocha, ni kwamba Libolo ilikuwa bora kuliko Simba SC. Mbaya zaidi, Libolo wameikuta Simba SC katika wakati mgumu, kama ambavyo nimeainisha hapo, wachezaji wengi majeruhi, wagonjwa. 
    Niliwahi kuandika, huyu babu Mfaransa amekuja katika wakati mbaya sana Simba SC, hajakuta timu, lakini anaonekana ni kocha mzuri, siyo tu kwa rekodi bali hata kile anachokifanya uwanjani.
    Anaweza kuondoka hata leo. Kama ataumia kupoteza ajira, hata Simba itaathirika kupoteza kocha hodari. Nidhamu ya wachezaji wa Simba SC wa sasa kwa kweli si nzuri, hilo nimekwishawahi kulielezea mara kadhaa.

    UONGOZI:
    Najaribu kutafuta kosa la uongozi wa Simba katika kuiandaa timu, kwa kweli silioni zaidi ya kuboronga katika usajili. Labda iwe kuna matatizo ya ndani sana.
    Baada ya kupoteza wachezaji muhimu akiwemo Patrick Mutesa Mafisango aliyefariki dunia na Kevin Yondan aliyehamia Yanga, tuliona wameletwa wachezaji wawili kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), beki Lino Masombo azibe pengo la Yondan na kiungo Patrick Kanu Mbivayanga azibe pengo la Mafisango.
    Walikuwa wachezaji wazuri tu, labda kama walikuwa wana mapungufu yenye kuhitaji marekebisho, lakini kabla ya Ligi Kuu kuanza, wakatemwa wote. Kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji, alisajiliwa Danny Mrwanda, akaachwa.
    Wakasajiliwa wachezaji watatu, mabeki Komanbil Keita kutoka Mali na Paschal Ochieng kutoka Kenya na mshambuliaji Daniel Akuffo kutoka Ghana. Kabaki Keita tu, wengine waliachwa baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu.
    Sasa dirisha dogo Simba SC ilimsajili nani, japo wa hapa hapa nyumbani? Ni kipa tu Abbel Dhaira kutoka Uganda, wakati siku chache baadaye ikamuuza Mganda Emmanuel Okwi, aliyekuwa akionekana kama mhimili mkubwa wa safu ya ushambuliaji ya timu.
    Na viongozi walionekana kujenga imani sana na wachezaji wao waliowapandisha kutoka timu ya vijana, akina Hassan Hatibu, Miraj Adam, Marcel Kaheza, Edward Chirstopher, Haruna Chanongo, Seseme, Singano, Mkude, Rashid Ismail, Miraj Madenge na wengineo.
    Sisi wa vyombo vya habari tulikuwa mstari wa mbele kuwastaajabu Simba, kwa nini wahangaike kusajili wachezaji wa kigeni kwa fedha nyingi, badala ya kupandisha wachezaji wao wa B, ambao wamekuwa wakizitoa nishai timu kubwa?
    Nasi tuna matatizo, tunavutiwa na kitu pale tu kinapofanya vizuri, lakini kikifanya vibaya hatukumbuki ubora wake. Mwandishi yule yule, aliyeandika kwa mbwembwe, kwa nini asajiliwe mchezaji wa kigeni kwa fedha nyingi, wakati wapo watoto wenye vipaji Simba B, leo anarudia rudia kumfananisha Chanongo na Emmanuel Okwi.
    Wapo miongoni mwetu wanaandika dhahiri kinazi, kwa mapenzi yao kwa Simba wanaguswa na timu inapofanya vibaya, hata wanasahau mwongozo wa kitaaluma, wanawalima kwa jazba viongozi wa timu yao, bila hoja. Viongozi waondoke.
    Kawaida yetu, kila siku ni afadhali ya jana na hii ni kwa sababu tunashindwa kutengeneza hoja za kutatua matatizo ya wakati uliopo na tunaona njia nyepesi ni mabadiliko, hata bila kufuatwa kwa utaratibu. Hili linaturudisha sana nyuma.
    Saa ngapi tunawapa watu fursa ya kujitazama mara mbili na kurekebisha makosa yao? Haitoshi kuwaambia watu walipokosea na kuwataka warekebishe makosa yao?
    Leo utarudia kutoa mifano ya Okwi. Lakini huyo hakuzaliwa na mpira mguuni, aliukuta duniani akajifunza, akaendelezwa na hata wakati analetwa Simba SC, hakuna aliyekuwa anamjua. 
    Mara ya mwisho niliwaona vijana wa Simba B Januari mwaka huu wakicheza na Azam iliyokamilika katika Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi na wakatolewa kwa mikwaju ya penalti katika siku ambayo wangeweza kushinda 2-1.   
    Uko wapi msingi wa kuwaendeleza wale vijana? Simba SC iliyoifunga Hearts Of Oak 2-0 Ghana mwaka 1974 haikuwa na mchezaji wa kigeni na mabao yalifungwa na Adam Sabu (marehemu) na Abdallah Kibadeni pale Accra.
    Simba SC iliyofika fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993 haikuwa na mgeni. Simba SC iliyoitoa Zamalek mwaka 2003 mgeni alikuwa Ramadhani Wasso pekee kutoka Burundi. 
    Sikatai, inawezekana uongozi wa Simba SC ukawa na matatizo, lakini vema kuwaambia mapungufu yao warekebishe makosa, kuliko kushinikiza mabadiliko. Sidhani kama ni busara kwa Mwandishi au chombo cha habari kuwa chanzo cha mgogoro katika soka yetu, kwani tutakuwa tunachangia kudumaa kwa mchezo huo nchini.
    Shabiki anaposoma Mwandishi, au Mhariri kaandika viongozi waondoke, huyo kesho lazima atakwenda kufanya fujo Msimbazi. Ipo haja ya kutumia kalamu zetu vizuri na kwa tahadhari, haswa wakati wa matatizo, wakati ambao watu wana jazba kama ilivyo hivi sasa Simba SC. Ni hayo tu. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: TUIHURUMIE SIMBA SC, TUSICHOCHEE KUNI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top