Alhaj Ismail Aden Rage; Hatima yake sasa ipo mikononi mwa Kamati ya Mgongolwa |
Na Boniface Wambura
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limepokea barua kutoka uongozi wa Simba ikielezea kutotambua mkutano ulioandaliwa na wanaodaiwa kuwa wanachama wake na kufanyika jana ukumbi wa Starlight, Dar es Salaam.
Vilevile katika barua hiyo uongozi wa Simba umeahidi kuitisha mkutano wa wanachama wake. Mkutano huo utaitishwa na Mwenyekiti wa Simba kwa mujibu wa katiba ya klabu hiyo.
Kutokana na hali hiyo, TFF imeitisha mara moja kikao cha Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji kinachoongozwa na Wakili Alex Mgongolwa kwa ajili ya kutoa mwongozo kwa matukio ya aina hiyo.
Hata hivyo, TFF tunasisitiza kwa wanachama wetu ikiwemo Simba kuwa wanachama wanapotaka kufanya uamuzi wowote ule wanatakiwa kuzingatia katiba na kanuni zilizopo.
Jana wanachama 698 wa klabu ya Simba leo walifikia uamuzi wa kuuondoa madarakani uongozi wa klabu yao na kuunda Kamati Maalum ya Muda, wakiwateua Zacharia Hans Poppe na Rahma Al Kharoos ‘Malkia wa Nyuki’ kuiongoza.
Katika Mkutano uliofanyika kwenye ukumbi maarufu wa Star Light Cinema, Dar es Salaam, wanachama hao walifikia uamuzi wa pamoja kuuondoa madarakani uongozi huo, kutokana na kile kilichoelezwa kushindwa kutekeleza majukumu yao na kuifikisha timu pabaya.
Pamoja na kuikabidhi timu kwa Hans Poppe, wanachama hao wamesema watakuwa bega kwa bega na viongozi hao wateule kuhakikisha wanafanikisha azma ya kurejesha hadhi na makali ya timu.
Awali ya hapo, mapema juzi, uongozi wa Simba SC ulitoa taarifa ya kuukana Mkutano wa jana kwamba ni batili na Mkutano Mkuu halali wa klabu hiyo, utafanyika baada ya Mwenyekiti wa klabu, Alhaj Ismail Aden Rage kurejea kutoka India anakotibiwa.
Lakini wanachama hao jana wamesema wameamua kufanya Mkutano huo kwa sababu uongozi umekuwa ukipiga chenga kufanya Mkutano na kulingana na hali ilivyo mbaya ndani ya klabu, wamechukua hatua hiyo ili kuinusuru klabu.
Alipoulizwa jana, Zacharia Hans Poppe kuhusu kuteuliwa kwake, kwanza alisema hana taarifa za Mkutano huo wala yaliyofikiwa.
“Sina taarifa na wala siafiki, kwa sababu hakuna mtu aliyeshauriana na mimi kabla, na pia wamefanya mambo kinyume na Katiba,”alisema Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
“Lazima wanachama wawe na subira, wasubiri Mwenyekiti arudi aitishe mwenyewe Mkutano, yeye mwenyewe (Mwenyekiti) alikwishasema ataitisha Mkutano, sasa kitu gani kinachowafanya wao wanakosa subira,”.
“Mbaya zaidi wamekwenda kufanya Mkutano wao na kufikia maamuzi yao, bila hata kunitafuta kuniuliza kwanza, sasa hii si ni dharau? Ina maana wao wanataka mimi nifanye wanavyotaka wao, mimi sitaki kuwa sehemu ya migogoro katika Simba,” alisema Hans Poppe.
Malkia wa Nyuki hakupokea simu alipopigiwa jana ili kuzungumzia uteuzi wake katika Kamati hiyo.
Hamkani si shwari sasa ndani ya Simba SC, kufuatia viongozi wawili wa Kamati ya Utendaji, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Hans Poppe aliyekuwa pia Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili kujiuzulu wiki mbili zilizopita.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Rage yuko India kwa matibabu na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Joseph Itangare ‘Kinesi’ aliyeteuliwa kukaimu Umakamu Mwenyekiti, sasa ndiye anakaimu Uenyekiti wa klabu.
Aidha, Baraza la Wazee kwa pamoja na Baraza la Wadhamini, wameunda Kamati Maalum ya kusimamia timu kuhakikisha inafanya vizuri katika wakati huu mgumu, chini ya Mwenyekiti, Malkia wa Nyuki.
Malkia wa Nyuki alianza vyema baada ya kuiongoza Simba SC kuilaza 2-1 Coastal Union katika mchezo wake uliopita na sasa anajiandaa kwenda kucheza mechi ya pili, dhidi ya Kagera Sugar mjini Bukoba wiki ijayo.
Simba SC ambao ni mabingwa watetezi, kwa sasa inazidiwa kwa pointi 14 na Yanga SC, inayoongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 48, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 37. Simba ya tatu.