Mrisho Ngassa; Mfungaji wa bao la pili la Simba SC |
Na Asha Saidi, Mwanza
SIMBA SC imelazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 na wenyeji Toto African kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni hii.
Kwa matokeo hayo, Simba SC inabaki nafasi ya tatu kwa pointi zake 35 baada ya kucheza mechi 21, nyuma ya Azam yenye pointi 43 na Yanga 49 kileleni.
Hadi mapumziko, timu hizo zilikuwa zimekwishafungana bao 1-1, mabao yote yakipatikana ndani ya dakika mbili, Toto wakianza na Simba SC wakisawazisha.
Bao la Toto lilifungwa na mshambuliaji Mussa Said dakika ya 25 kwa shuti la mbali baada ya Wana Kishamapanda kufanya shambulizi kali la kushitukiza.
Rashid Ismail aliisawazishia Simba SC dakika ya 26 baada ya kuuwahi mpira uliorudi kufuatia kutokea piga nikupige langoni mwa Toto. Simba SC walisawazisha bao hilo kwa shambulizi la kwanza tu, wakitoka kuanza mpira baada ya kufungwa.
Kipindi cha pili, Simba SC waliingia na kasi zaidi sambamba na kufanya mabadiliko, Mrisho Khalfan Ngassa akiingia kuchukua nafasi ya Rashid Ismail dakika ya 52.
Hakika Ngassa aliibadilisha mno Simba, kwani alionekana dhahiri kutengeneza mashambulizi mengi ya hatari.
Jitihada za Ngassa zilizaa matunda dakika ya 62 baada ya kufumua shuti la umbali wa mita 35, ambalo lilimshinda kipa wa Toto, Eric Ngwengwe.
Hata hivyo, Toto walizinduka baada ya bao hilo na kuanza kushambulia nao.
Selemani Kibuta aliisawazishia Toto dakika ya 72 baada ya mabeki wa Simba SC kujichanganya na kumpa mwanya mshambuliaji huyo wa Toto kufunga, aliyeingia kipindi cha pili kusawazisha.
Katika mchezo huo, kikosi cha Simba SC kilikuwa; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’/Haruna Shamte dk42, Miraj Adam, Shomary Kapombe, Hassan Khatib, Jonas Mkude/Ramadhani Kipalamoto dk 46, Amri Kiemba, Abdallah Seseme, Rashid Ismail/Mrisho Ngassa dk 52, Ramadhan Singano ‘ Messi’ na Haruna Chanongo.
Toto African; Eric Ngwengwe, Eric Mulilo, Robert Magadula, Evarist Maganga, Hamisi Msafiri, Mussa Said, Emanuel Swita/Mohamed Neto dk 67, Heri Mohamed/Selemani Kibuta dk55, James Magafu, Mohamed Jingo na Eric Kyaruzi.