Mrisho Ngassa |
Na Ezekiel Kamwaga, Kwanza Sul, Angola
KLABU ya Recreativo de Libolo ya Angola, imewasilisha rasmi maombi ya kumsajili winga wa Simba SC, Mrisho Khalfan Ngassa, lakini klabu yake imeshitukia ofa hiyo.
Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Augusto Correia, aliwasilisha maombi hayo jana kuelekea mechi ya marudiano ya Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika baina ya timu hizo, mara tu baada ya SImba kutua nchini humo.
SIMBA ilitua nchini Angola jana asubuhi na moja kwa moja wenyeji wao, Libolo wakawapeleka katika mji wa Calulo uliopo katika jimbo la Kwanza Sul, umbali wa dakika 35 kwa ndege kutoka mji mkuu wa Angola, Luanda ambako Simba ilifika majira ya saa nne asubuhi.
Hata hivyo, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba ambaye ndiye kiongozi mkuu wa klabu katika timu nchini Angola, Zacharia Hans Poppe, aliwakatalia Libolo kujadili chochote kuhusu Ngassa hadi baada ya mechi kesho.
Katika mazungumzo yake na Poppe, Correia alisema wanataka kuzungumza na uongozi wa Simba, lakini Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Usajili akasema inabidi Libolo wasubiri kwanza mechi ichezwe.
Pamoja na Libolo kuonyesha nia ya kumsajili Ngassa, lakini hakuna hakika kama mchezaji mwenyewe ataipapatikia ofa hiyo, kwani tayari amekwishakataa ofa kadhaa za kucheza nje, ikiwemo APR ya Rwanda na El Merreikh ya Sudan.
Ngassa ambaye amewahi kufanya majaribio West Ham United ya England na Seattle Sounders ya Marekani, anaonekana kama mtu ambaye ameridhika kucheza hapa hapa nyumbani.