Kikosi cha Mgambo; Azam, Simba na Yanga wajipange |
Na Baraka Mpenja
SIMBA SC na Yanga pamoja na Azam, wote wana mechi na Mgambo Shooting katika hatua hii ya lala salama ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. sasa wajipange sawasawa, maana Mgambo wamepania.
Shavu wanalopewa na mashabiki wa kandanda ndani ya jiji la Tanga "waja leo waondoka leo" ndio siri ya Maafande wa kupiga kwata wa Mgambo Shooting kuendelea kupigana kufa na kupona ili kukwepa panga la kuporomola daraja katika msimu huu wa ligi kuu soka Tanzania bara.
Akizungumza leo kwa kujiamini, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Antony Mgaya amesema kuwa wanajipanga kufanya maajabu mechi zilizosalia na kujihakikishia nafasi ya kushiriki lligi kuu msimu ujao.
Mgaya amejigamba kuwa kocha wao Mohamed Kampira anafanyia kazi makosa yote yaliyojitokeza mechi za nyuma na sasa anaumiza kichwa kupata pointi nyingi mechi zilizosalia.
"Ukiangalia msimamo wa ligi kuu kwa sasa kabla ya mechi za leo, sisi tupo nafasi ya tisa na pointi 24, tuko mbele ya timu tano zinazowania kukwepa kisu cha kushuka daraja, tunapanga makombora na madalagu yetu yote kuhakikisha ngwe iliyosalia tunapata ushindi na kuwa salama". alijigamba Mgaya.
Akizungumzia mikakati ya uongozi wa timu, Mgaya alisema wanajitahidi kuwajibika kwa sehemu yao ikiwa ni pamoja na kukidhi mahitaji ya wachezaji wao kwa maana ya mishahara, posho na vifaa vya michezo ili kujenga hali ya hewa nzuri ndani ya klabu.
"Tunajua fika kuwa wachezaji wanahitaji kuwa karibu nao katika kazi yao, sisi kama viongozi tunahakikisha mambo yanakwenda swadakta, na ndio maana wachezaji wameahidi kupambana katika vita hii ya kubakia ligi kuu na kuanza mipango ya msimu ujao kwa kiwango cha juu". Aliongeza Mgaya.
Pia kiongozi huyo alisifu shangwe na nderemo wanazopata kwa mashabiki wa mchezo wa soka jijini Tanga kila wanaposhusha daluga zao dimbani kuhitaji pointi tatu muhimu.
Mgaya alisema hakuna utofauti kati yao na Coastal union, wote wanashangiliwa kwa nguvu sawa kitendo kinachoonesha uzalendo miongoni mwa wana Tanga, "waja leo waondoka leo".
Kufuatia baadhi ya timu kuwatuhumu wachezaji wao kuwa na mapenzi ya timu kubwa na kucheza chini ya kiwango kila wanapokutana nazo, Mgaya alisema katika kikosi cha Mgambo hakuna kitu kama hicho, wachezaji wote wanacheza kwa kujituma wakitambua kuwa ni ajira yao.
Aidha katibu huyo amesema kwa sasa wapo Tanga na wanapiga jalamba la kufa mtu wakipanga kikosi cha mashabulizi kwa ajili ya mechi zao.
Mgambo shooting ni moja kati ya timu zilizopanda kucheza ligi kuu soka Tanzania bara msimu huu uliopo ukingoi sambamba na Wajela jela Tanzania Prisons pamoja na Polisi Morogoro.
Tangu waanze mitanange ya ligi kuu, wameonekana kucheza kama timu huku wakipambana kufa na kupona licha ya kuwepo kwa mapungufu machache ya kiuchezaji ambayo husababishwa na ugeni wao katika michuano hii mikubwa nchini Tanzania