KILA mtu anasema kulingana na upeo wake katika sakata la hatari ya Tanzania kufungiwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na hii kwa sababu, mpira wa miguu unapendwa na watu wengi sana. Wamo weledi sana, mbumbumbu kupita kiasi, wenye akili timamu na machizi. Wote wapenzi wa soka.
Lakini wengi hawajui athari zake na ndiyo maana hata pande mbili zinazovutana, Serikali na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zinaendelea kuvutana kutokana na kusoma hisia za watu na mitazamo yao juu ya hili.
Kila upande unajiona unaungwa mkono na unajiona uko sahihi, kiasi kwamba wanashindwa kutafakari kwa kina zaidi juu ya sakata hilo na kufikiria zaidi namna ya kulipatia ufumbuzi, zaidi tu ya kutaka kuonyeshana nani zaidi.
Sikio halizidi kichwa, viongozi waliopo madarakani TFF wasidhani kama serikali itaamua kupambana nao bila kujali athari zozote zitakazoikumba soka ya nchi hii watasimama. Hawawezi. Mgogoro wa Katiba, hilo ndilo somo.
Serikali inasema TFF hawakufuata taratibu katika kuipitisha Katiba yao. Kweli. TFF wanasema wanaingiliwa na Serikali, jambo ambalo lipo kinyume na mwongozo wa FIFA na adhabu yake ni kufungiwa.
Ni kweli Serikali inaiingilia TFF katika hili? FIFA imetoa mamlaka kamili kwa wanachama wake, yaani bodi za nchi za soka, zijiendeshe zenyewe kwa utaratibu uliowekwa (na FIFA) bila kuingiliwa. Sahihi. Lakini TFF katika utaratibu wake, imejiingiza yenyewe serikalini kwa kujisajili na kuweka utaratibu wa kujisajili na kupitisha Katiba zake kupitia serikali.
Serikali tayari ina mwongozo wa utaratibu wa uendeshwaji wa zoezi la ubadilishwaji wa Katiba ndani ya TFF, ambao safari hii TFF wenyewe wameukiuka. Kwa hivyo, serikali kwa kutambua umuhimu wa ushirikishwaji wao, wameamua kutilia mkazo utaratibu unaotambulika kikatiba ufuatwe.
Wameagiza TFF iitishe Mkutano Mkuu kujadili Katiba mpya. TFF haitaki, inasema imekwishapitisha katiba yake kwa njia ya waraka, jambo ambalo kwenye Katiba yao inayotambulika serikalini halipo. Nani yupo sahihi hapa?
Kilichopo au kinachokuja ni TFF kuwatisha Serikali kwamba, ikiendelea kusistiza masharti yake, Tanzania itafungiwa. Hapo ndipo kwenye ngoma. Bado siamini kama wapo watu ndani ya TFF kwa maslahi yao binafsi wako tayari kuona nchi hii inaondoka kwenye ramani ya soka ya kimataifa. Sitaki kuamini.
Jana Rais wa TFF amezungumzia sakata hilo na kuwataka wadau wa mchezo huo kuwa watulivu kwa vile tofauti zilizojitokeza kati ya Shirikisho na Serikali zitamalizwa kwa taratibu za mpira wa miguu.
Alisema nia ya TFF ni kuhakikisha FIFA haiifungii Tanzania, kwani tayari Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara alishaahidi kuwepo kikao kati yake na viongozi wa TFF kitakachofanyika Jumanne (Machi 19 mwaka huu).
“Suluhu itapatikana kwa mazungumzo kati ya Wizara na TFF. Naamini suala hili tutalimaliza baada ya kikao cha Machi 19 ambacho kimepangwa na Waziri kutokana na maombi ya TFF,” alisema Rais Tenga na kuongeza kuwa tatizo lilianzia kwenye mchakato wa uchaguzi ambao umesimamishwa na FIFA.
FIFA ilisimamisha Mkutano Mkuu wa uchaguzi baada ya baadhi ya wagombea walioenguliwa kulalamika, na yenyewe kuahidi kutuma ujumbe wa kushughulikia suala hilo.
Rais Tenga amesema lisingetokea tatizo hilo, TFF tayari ilishaitisha Mkutano Mkuu ambao ungefuatiwa na uchaguzi. Lakini kwa vile FIFA ndiyo iliyosimamisha mkutano huo, TFF inalazimika kusubiri hadi FIFA itakaposhughulikia suala hilo na kutoa maelekezo ikiwemo lini mkutano ufanyike.
Amesema kwa kuamini tatizo hilo litamalizwa ndani ndiyo maana TFF hadi sasa haijapeleka FIFA maagizo ya Waziri Dk. Fenella ya kutengua marekebisho ya Katiba ya TFF ya mwaka 2012, kuitisha Mkutano Mkuu wa marekebisho ya Katiba na Mkutano Mkuu wa Uchaguzi, kwani ingefanya hivyo Tanzania ingefungiwa mara moja.
TFF inasisitiza kuwa FIFA ilijua tatizo la Serikali kutoa maagizo kwake kupitia vyombo vya habari, hivyo kumuandikia Rais Tenga na kueleza msimamo wake iwapo itabainika kuwa Serikali imekuwa ikiingilia uendeshaji wa shughuli za mpira wa miguu.
Uhalali wa kuwepo kwa barua ya FIFA kwenda kwa Rais Tenga juu ya suala hilo ulihojiwa pia na mwandishi wa Reuters, Brian Homewood baada ya kusoma kupitia vyombo vya habari nchini kuwa Shirikisho hilo huenda likaifungia Tanzania ikibainika Serikali inaingilia shughuli za TFF.
Lakini tayari FIFA imekwishatuma barua TFF kwa mujibu wa TFF wenyewe, ikisema kupitia vyombo vya habari imesikia Serikali inaiingilia TFF, hivyo inafanyia uchunguzi suala hilo na ikigundua ni kweli, itachukua hatua, ambayo ndiyo hiyo kufungiwa.
Je, tunajua athari za kufungiwa kwa wale ambao wako tayari tufungiwe na FIFA? Soka ni ajira kwa vijana wengi hivi sasa na wengi wako kwenye hatua za kujifunza mchezo huo kwa matarajio iwakomboe kimaisha.
Tumekuwa tukilia kwa muda mrefu watu waje kuwekeza kwenye soka yetu, watu wameanza kuja. Tazama ule uwekezaji mkubwa wa Alhaj Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake pale Chamazi, yalipo makao makuu ya Azam FC.
Kama tutafungiwa ni hasara kiasi gani tutakuwa tumeiingiza familia ya Bakhresa na kaisi gani Tanzania itapoteza. Tukifungiwa, akina Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaocheza TP Mazembe ya DRC pamoja na wachezaji wote wa Tanzania waliopo nje watarudi.
Makampuni yote yaliyowekeza fedha zake nyingi kwenye soka yetu wakiwemo Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), wadhamini wa Taifa Stars, Simba na Yanga yatabaki kufanya nini? Hata baadhi ya watu waliojiingiza kwenye soka siku za karibuni, kama Yussuf Manji wanaweza kubaki kweli, ikiwa soka yetu haitavuka mipaka?
Zipo klabu za nje zimeonyesha nia ya kushirikiana na klabu zetu hapa kama Sunderland ya England, inayotaka kuanzisha uhusiano na Simba SC, zoezi ambalo lilimhusisha hadi Mheshimiwa Rais, Jakaya Kikwete, je tukifungiwa zitahitaji uhusiano na sisi wa nini ikiwa hatupo kwenye familia ya soka duniani?
Ipo haja, kwa yeyote anayehusika katika sakata hili, hususan Serikali na viongozi wenyewe wa TFF akaweka mbele maslahi ya taifa. Akameza fundo la uzalendo moyoni mwake na kujivua mkufu wa ubinfasi shingoni mwake. Wasalam.