Samatta kulia na Ulimwengu kushoto |
Na Prince Akbar
WASHAMBULIAJI mahiri ya timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emanuel Ulimwengu wanaochezea TP Mazembe ya DRC, wameahidi kupigana kufa na kupona kuiwezesha timu hiyo kuwafunga Morocco Jumapili katika mchezo wa Kundi C, kuwania tiketi ya kucheza Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil.
Wawili hao waliowasili nchini Jumatatu jioni kutoka Lubumbashi, DRC na kujiunga na wachezaji wenzao tayari kwa maandalizi ya kuikabili Morocco wamesema wamekuja nchini kwa ajili ya kazi moja tu, kulibeba taifa lao
Wachezaji hao, ambao ni tegemeo kubwa katika TP Mazembe wamewahakikishia Watanzania ushindi Jumapili hii na kuwataka wajitokeze kwa wingi kuishangilia timu yao ya Taifa.
Akizungumza mara baada ya kuwasili, Samatta alisema ushindi dhidi ya Morocco ni lazima, hivyo Watanzania wasiwe na hofu na timu yao na wao wako tayari kuliongoza jahazi hilo la ushindi.
“Tumekuja kuungana na wachezaji wenzetu wa Timu ya Taifa, tumekuja kuhakikisha timu yetu inashinda na tuna kila sababu ya kushinda maana tunacheza nyumbani,” alisema Samatta ambaye aliifungia Tanzania bao la ushindi dhidi ya Cameroon mapema mwaka huu.
Alisema kuwa wao wako fiti na hawana tatizo lolote na wanajiunga na kambi usiku huo huo waliowasili na kuanza mazoezi kama ratiba ilivyo pangwa na hivyo watanzania wajiandae kushangilia ushindi.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro lager, ipo kambini tangu Jumamosi na tayari wachezaji wote 23 walioitwa wameripoti kambini.
Kocha wa timu hiyo, Mdenmark Kim Poulsen amekwishasema kuwa hana wasiwasi na Morocco kwani ameshawasoma na kuona mchezo wao wakati wa Kombe la Afrika na juzi wakati Morocco ilicheza na Mali kwa hivyo anajua namna ya kuwaandaa wachezaji wake kukabiliana nao.
Taifa Stars iko katika kundi moja na Ivory Coast, Morocco na Gambia huku Ivory Coast ikiongoza kwa pointi nne, Tanzania ya pili na pointi tatu, Morocco pointi mbili na Gambia pointi moja.
Ushindi katika mechi hii utaiweka Stars katika nafasi nzuri ya kufuzu Fainali za kwanza za Kombe la Dunia.