GWIJI wa soka duniani, Edison Arantes do Nascimento maarufu kama Pele, aliwahi kusema; “Success is no accident. It is hard work, perseverance, learning, studying, sacrifice and most of all, love of what you are doing or learning to do”.
Alikuwa akimaanisha, mafanikio hayaji kama ajali. Yanatokana na kazi ngumu, uvumilivu, kujifunza, kujitoa mhanga na zaidi ya yote kupenda unachokifanya au unachojifunza.
Nenda kwa wazee wa siku nyingi pale Kariakoo watafute na waulize siri ya utajiri wa Alhaj Said Salim Awadh Bakhresa, watakuambia alisota. Aliumia ili kutimiza malengo yake na sasa watoto wake wanaishi maisha mazuri mno, ambayo baba yao katika ujana wake hakuishi.
Siri ya mafanikio ni kujitoa na kuyatengeneza, kamwe hayatakuja kama ajali. Vivyo hivyo, katika soka, wanaofanikiwa ni wale ambao wanafanya kazi ngumu, wanavumilia, wanajifunza, wanajitoa mhanga na wanapenda wanachokifanya. Hawasukumwi.
Kama wewe ni mchezaji, ukiona mazoezi ni adhabu, basi huwezi kufika popote. Kama wewe ni mchezaji ukivimba kichwa na ukaanza kudharau viongozi wako, walimu wako, umekwisha. Kama wewe ni mchezaji hautakuwa mvumilivu, hauwezi kufika popote.
Nitatoa mfano mmoja; Nwankwo Kanu ni miongoni mwa wanasoka wa Afrika waliofanikiwa sana- lakini katika siku za mwanzo za maisha yake ya soka alilazimika kucheza bure, baadaye kwa ujira mdogo katika klabu za kwao, Nigeria za Federation Works na Iwuanyanwu Nationale, ambazo zilimfanya aiwe timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya nchi hiyo.
Huo ndiyo ukawa mwanzo wa mafanikio yake, baada ya mashindano ya Kombe la Dunia la U17 mwaka 1993 nchini Japan, Kanu alinunuliwa na AFC Ajax ya Uholanzi, mwaka 1993 kwa Euro 207,047 wakati huo hiyo ni klabu kubwa na inayotikisa Ulaya.
Wanasoka wote walioogelea kwenye fedha Ulaya, walipitia tabu hapa Afrika. Thomas Ulimwengu alivumilia ugali na maharage kila siku, kunywa maji ya bomba yaliyochemshwa tu katika akademi ya TSA pale Uwanja wa Karume kwa miaka isiyopungua miwili.
Alikuwa analala sehemu ya vyo kwenye zile hosteli- lakini alikuwa ana malengo ambayo leo yameanza kutimia akiwa mshambuliaji tegemeo wa klabu ya Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na siku moja anaweza kucheza Ulaya, kama ataendelea hivi na hatavimba kichwa.
Analala sehemu nzuri mno. Anatembelea gari zuri. Anafanya mazoezi katika mazingira mazuri. Analipwa vizuri. Anafurahia maisha kwa ujumla na amekwishasahau msoto wa Karume.
Wanasoka wengi wa Tanzania huwa wanakuwa na mwanzo mzuri, lakini wakipata mafanikio kidogo ya awali ikiwemo kusajiliwa Simba na Yanga au kuchezea timu ya taifa, wanajiona wamemaliza na kweli huo ndiyo unakuwa mwisho wao.
Hawafiki popote, wakati wanaweza kufika mbali na hata kucheza timu kubwa Ulaya na kulipwa fedha nyingi kama wanavyolipwa wenzao. Mtazame Mwinyi Kazimoto anaelekea wapi. Sasa anawekwa kundi moja na wachezaji walioshindikana akina Amir Maftah, Haruna Moshi ‘Boban’ na Juma Nyosso.
Hakuna haja ya kupindisha maneno; akina Boban wameshindikana. Wameshindikana na walimu wengi. Watu wamekwishawachukulia sana kibinadamu kulingana na mapungufu yao, lakini imeshindikana. Sasa Kazimoto ambaye alikuwa anainukia vizuri, ameingizwa katika kundi hilo.
Kocha Mfaransa wa Simba SC, Patrick Liewig hamtaki kwenye kikosi chake pamoja na ‘makungwi’ wake akina Boban, Nyosso na Maftah. Katika mechi dhidi ya Morocco, Mwinyi alicheza chini ya kiwango na akatolewa baada ya dakika 45 tu, nini kinachofuata?
Nampongeza Athumani Iddi ‘Chuji’ ametulia, amebadilika kweli. Sijui hapo baadaye tena. Sasa anacheza mpira na bidii na mazoezi na ndiyo maana anapangwa kuanzia Yanga hadi Taifa Stars. Hata asicheze kwa matarajio ya kwenda Ulaya tena, lakini amalize vizuri kwa heshima. Mwinyi anakwenda wapi?