Na Daudi Julian, Morogoro
MAFUNZO elekezi ya siku mbili ya sheria 17 za soka yanatarajia kufanyika machi 23 na 24, mwaka huu, mjini Morogoro.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY, Mratibu msaidizi wa mafunzo hayo, Fredrick Luunga alisema mafunzo hayo yatashirikisha wadau mbalimbali wa mchezo wa soka katika Manispaa ya Morogoro na kwamba yatafanyika katika ukumbi wa Mango.
Luunga aliwataja baadhi ya wadau hao kuwa ni waamuzi wa mchezo huo, makocha, viongozi wa klabu, wachezaji, waandishi wa habari za michezo pamoja na mashabiki wa kawaida.
Alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wadau hao kuzijua ipasavyo na kuzitafsiri vema sheria hizo.
Mratibu huyo alisema mafunzo hayo yanafuatia utafiti wa muda mrefu ambao amedai umebaini kuwa wadau wengi wa soka nchini hawazijui ipasavyo sheria za mchezo huo na hivyo kuwa chachu ya vurugu katika mechi mbalimbali za soka.
“Maandalizi kwa ajili ya mafunzo haya yanakwenda vizuri na tayari tumeshaanza kutoa fomu kwa washiriki”, alisema.
Luunga alisema wakufunzi katika mafunzo hayo ni wanaotambuliwa na chama cha waamuzi wa mpira wa miguu nchini (FRAT) ambao amedai wana uwezo mkubwa wa kutafsiri sheria hizo.
Mratibu huyo ametoa wito kwa wadau wa soka katika manispaa ya Morogoro kujitokeza kwa wingi kwa lengo la kuchukua mafunzo hayo.