Azam FC, Mashujaa wa Taifa |
Na Mahmoud Zubeiry
WAWAKILISHI wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika, wanatarajiwa kutua nchini kesho asubuhi kufuatia ushindi wa mabao 2-1 jana ugenini dhidi ya wenyeji Barrack Young Controllers katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Pili ya michuano hiyo uliofanyika kwenye Uwanja wa Antonette Tubman Monrovia, Liberia.
Kwa matokeo hayo, Azam sasa itahitaji hata sare tu ili kusonga mbele, Raundi ya Tatu na ya mwisho ya mchujo kabla ya hatua ya makundi.
Kocha Muingereza wa Azam FC, Stewart Hall akizungumza kwa simu na BIN ZUBEIRY kutoka Monrovia leo, amesema kwamba amefarijika na ushindi huo, lakini amesema hawatabweteka bali watajipanga kushinda pia mchezo wa marudiano.
“Tulistahili ushindi, tulicheza vizuri, tulipoteza nafasi kipindi cha kwanza, wakatangulia kufunga, lakini kipindi cha pili tulijirekebisha na tukapata mabao mawili muhimu, nia yetu ni kufika mbali,”alisema Stewart.
Tayari wapenzi na mashabiki wa Azam Dar es Salaam wanajipanga kwa ajili ya kuifanyia mapokezi makubwa timu yao itakapowasili kesho.
Shujaa wa Azam FC jana alikuwa ni Seif Abdallah Karihe aliyefunga bao la ushindi dakika ya 90, zikiwa ni dakika 10 tangu aingie uwanjani kuchukua nafasi ya Kipre Tchetche, kufuatia kazi nzuri ya Mzanzibari mwenzake, Khamis Mcha ‘Vialli’.
Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Farouk Mohamed kutoka Misri, hadi mapumzikko, B.Y.C. walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililofungwa na Junior Barshall dakika ya 44 na Azam wangeweza kuondoka uwanjani baada ya dakika 45 za kipindi cha kwanza wakiwa wana mabao, iwapo wangetumia vizuri nafasi nzuri takriban sita walizopata.
Kwa muda mrefu kipindi cha kwanza, B.Y.C. walikuwa wanacheza kwa kujihami zaidi wakiwategeshea mitego ya kuotea wachezaji wa Azam FC na kipindi cha pili Azam FC baada ya kupata mawaidha ya kocha wao, Muingereza Stewart Hall walirejea uwanjani wamebadilika na kufanikiwa kusawazisha bao.
Alikuwa ni kiungo wa kimataifa wa Kenya, Humphrey Mieno aliyeifungia bao la kusawazisha Azam FC na sasa Azam inatarajiwa kurejea nchini kesho na mchezo wa marudiano utafanyika wiki mbili zijazo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, kikosi cha Azam FC kilikuwa; Mwadini Ally, Himid Mao, Waziri Salum, David Mwantika, Joackins Atudo, Ibrahim Mwaipopo aliyempisha Abdi Kassim ‘Babbi’ dakika ya 68, Humphrey Mieno, Kipre Balou, Khamis Mcha ‘Vialli’, John Bocco ‘Adebayor’ aliyempisha Jabir Aziz dakika ya 85 na Kipre Tcheche aliyempisha ‘mshindi wa mechi’, Seif Abdallah Karihe dakika ya 80.
Wakati huo huo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeipongeza Azam kwa ushindi huo.
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura amesema kwamba mechi hiyo dhidi ya Barrack Young Controllers II ilichezwa jana jijini Monrovia, na timu hizo zitarudiana wikiendi ya Aprili 6 au 7 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Amesema ushindi huo unaiweka Azam chini ya kocha wake Stewart John Hall katika mazingira mazuri ya kusonga mbele baada ya mechi ya marudiano. Bila shaka ushindi wa timu ya Azam pamoja na mambo mengine umechangiwa na klabu hiyo kujipanga vizuri.
Hata hivyo, amesema ushindi huo bado ni changamoto kwa wachezaji, benchi la ufundi na uongozi wa Azam kuhakikisha unajipanga vizuri kwa mechi ya marudiano kwa vile mpira wa miguu una matokeo ya aina tatu; kushinda, kutoka sare au kufungwa.
Msafara wa timu ya Azam unaoongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Blassy Kiondo unatarajiwa kurejea nchini kesho alfajiri kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Nairobi.