Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji kulia akizungumza na Waandishi wa Habari jana Jangwani. Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora, Mh. George Mkuchika. |
Na Mahmoud Zubeiry
MWENYEKITI wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Alhaj Yussuf Mehboob Manji amesema kwamba ukame wa mabao katika klabu hiyo hivi sasa unamnyima usingizi haswa akilifikiria deni la kufungwa 5-0 na wapinzani wao wa jadi, Simba SC.
Manji; 5-0 zinaniumiza kichwa |
Manji alisema kwamba amekwishazungumza na Benchi la Ufundi, chini ya kocha Mkuu, Mholanzi Ernie Brandts ambalo limemuahidi kulifanyia kazi tatizo hilo.
“Benchi la ufundi linafanyia kazi tatizo hilo, lakini hatuwezi kuona matunda yake ndani ya siku mbili, itachukua muda, ila kwa kweli inanichanganya sana,”.
“Sisi viongozi tumefanya juhudi zetu kusajili wachezaji wazuri na benchi zuri la Ufundi, tumeleta kocha bora, wachezaji wanaishi vizuri, wanapata maslahi mazuri. Sasa iliyobaki ni wao wafanye kazi,”.
“Lakini tunakwenda mechi nne sasa, timu inashinda bao moja, moja, timu tumeipeleka Ulaya, Uturuki kufanya kambi, inarudi hapa, haionyeshi tofauti na timu nyingine,”.
“Tunapata bao dakika ya sabini na…, tukipata dakika ya thelathini na…, inakuwa kucheza kwa wasiwasi hadi mpira uishe, sasa kwa nini. Inatakiwa tuashinde goli tatu, ukishinda goli tatu au zaidi, mpinzani akikutana na wewe anafikiria kupunguza iwe mbili, sasa kwa kweli inachanganya,”alisema Manji.
Akizungumzia mustakabali wa klabu kwa ujumla, Manji alisema wanafikiria kuanzisha akademi nzuri ya klabu hiyo katika mfumo ambao utahusisha matawi ya klabu hiyo mjini Dar es Salaam.
Alisema wako kwenye mchakato wa kuanzisha mashindano ya Kombe la Yanga, litakaloshirikisha timu za vijana za matawi na katika mechi za mashindano hayo, kocha atakwenda kuchagua wachezaji wa kuingia akademi.
Ameyataka matawi ya Yanga Dar es Salaam kuanza mchakato wa kuunda timu imara za vijana ili kusaidia kupatikana kwa wachezaji wa kuingia akademi.
Kuhusu ujenzi wa Uwanja wa kisasa, Manji alisema mchakato unaendelea vizuri na Juni zoezi litaanza kama alivyoahidi.
Alisema kuanzia sasa mali zote za Yanga zitakuwa zinasimamiwa na Baraza la Wadhamini, alilolizindua jana, linaloundwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora, Mh. Kapteni George Huruma Mkuchika, Balozi Ammy Mpungwe, Injinia Francis Mponjoli Kifukwe na Mama Fatuma Karume.
Alisema kwa mujibu wa Katiba, bado kuna nafasi za watu watatu katika Baraza hilo, ambao watateuliwa baadaye.
Aidha, Manji alisema pamoja na dhamira ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mapema, lakini anataka kulipa kisasi cha 5-0 ambazo Yanga ilifungwa mwaka jana na Simba SC katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu, wakati huo Mwenyekiti akiwa Wakili Lloyd Baharagu Nchunga.
Yanga SC inaongoza Ligi Kuu kwa sasa kwa pointi zake 48, baada ya kucheza mechi 20, ikifuatiawa na Azam yenye pointi 37 katika nafasi ya pili, wakati mabingwa watetezi, Simba SC wana pointi 34 katika nafasi ya tatu, zikiwa zimebaki mechi sita kuhitimisha msimu huu wa Ligi Kuu.