Na Mahmoud Zubeiry
YANGA SC inafanya vizuri kwenye soka kwa sasa. Inatisha. Lakini katika ndondi, imefulia. Hiyo inafuatia mabondia maarufu, ambao wamekuwa wakiiwakilisha klabu hiyo ulingoni kwa muda mrefu, kudundwa usiku wa leo kwenye ukumbi wa DDC Magomeni Kondoa, Dar es Salaam.
Hao si wengine, bali Joseph Marwa ‘Hungry Lion’ na Maneno Oswald ‘Mtambo wa Gongo’, ambao wakati fulani waliwafurahisha mno wana Yanga baada ya kumpiga bondia wa mahasimu wao wa jadi, Simba SC, Rashid ‘Snake Boy’ Matumla.
|
Kaseba kulia akimtupia konde Maneno |
|
Konde la Maneno limetua kweye kichwa cha Kaseba |
|
Maneno amepangua konde la Kaseba |
|
Wanaume wanashikana |
Wakati Marwa alikalishwa chini katika raundi ya mwisho ya pambano la raundi sita uzito wa juu (Heavy) na bondia kijana mdogo, Alphonce Mchumia Tumbo, Mtambo wa Gongo alimaliza raundi zote 10 katika pambano la uzito wa Super Middle kwa taabu na kupoteza kwa pointi mbele ya Japhet Kaseba.
|
Konde la Maneno limetua kwenye kidevu cha Kaseba |
Marwa ndiye aliyeanza kuadhibiwa, baada ya kupanda ulingoni katika pambano la pili kuelekea mwisho. Alianza vizuri raundi tatu za awali, akikabiliana vyema na mpinzani wake huyo, lakini baada ya hapo, alizidiwa ‘vibaya’.
Alionekana kutumia uzoefu kwa kumbana zaidi mpinzani wake, kuliko kupigana ili kujitahidi angalau amalize pambano na akafanikiwa kufika raundi ya mwisho, lakini hakuweza kuhimili vishindo vya kijana mwenye ngumi nzito hadi kengele ipigwe.
Zikiwa zimesalia sekunde 16 kengele ya kumaliza pambano ipigwe, Marwa alikaa chini baada ya kukutana na ngumi kali ya mpinzani wake. Alijikokota kuinuka, lakini akarudi chini tena na refa Anthony Rutta akamaliza pambano.
Hiyo ilikuwa mara ya pili kwa Marwa kukaa, awali sekunde ya 11 ya dakika ya pili katika raundi hiyo, alikalishwa tena, lakini akajikokota kuinuka na kuendelea.
Marwa alimpongeza mpinzani wake kwa ushindi huo na kusema pamoja na umri kumtupa mkono, lakini anaamua kuendelea kupigana mara moja moja, ili kuwapa changamoto vijana.
“Nimeonyesha mimi ni bondia bora, nimepigana na kijana mdogo na nimemtoa jasho, watu wameona. Kwangu hii ni ushindi tosha. Nimempa mazoezi ya kutosha kijana, ambayo sidhani kama anaweza kuyapata hata kwa vijana wenzake,”alisema Marwa.
Pambano la siku leo lilikuwa kati ya Maneno na Kaseba na ndilo lililovuta wengi katika ukumbi huo mkongwe. Maneno alikuwa wa kwanza kupanda ulingoni na kwenda kurithi kona ya mbabe wa Marwa, bluu na Kaseba akafuatia kwenye kona nyekundu.
Pambano lilianza kwa kasi kwa mabondia wote kurushiana ngumi kali na ikaonekana kama litaendelea kuwa la vuta nikuvute hadi mwisho.
Hata hivyo, baada ya raundi mbili, Mtambo wa Gongo ‘ulitepeta’ na kuanza kufanywa gunia la mazoezi na Kaseba.
|
Kaseba akimuadhibu Maneno |
|
Wanaume wakipambana, Maneno na Kaseba |
|
Refa Anthony Rutta akimuinua juu mkono Kaseba kumtangaza mshindi wa pambano |
|
Mama yake Maneno akicheza wimbo wa Saida Karoli, Kasiki wakati mwanawe akipanda ulingoni |
|
Refa Anthony Rutta akimfuta damu Maneno, baada ya kuchanwa juu ya jicho la kulia na Kaseba raundi ya saba |
Hakuna aliyetarajia japo Maneno atafika raundi ya saba, lakini mkongwe huyo alitumia uzoefu wake na maarifa mengi, kuhakikisha hakai chini hata mara moja. Alifanikiwa.
Kuanzia raundi ya tano, Maneno alikuwa akirejea kwenye kona yake huku akipepesuka na katika raundi ya nane alitaka kwenda kwenye kona ya kupumzikia, kutokana na kulewa makonde ya ‘Rasta’, lakini akaelekezwa na kwenda kwenye kona yake.
Maneno alishangaza wengi kuanzia raundi ya tisa, baada ya kurejea na nguvu mpya, akipigana kwa ukakamavu kama si yule ambaye aliondoka amelewa kiasi cha kusahau kona yake randi ya nane.
Mabondia hao walipigana kwa kujibizana masumbwi katika raundi hizo mbili za mwisho hadi kengele ilipolia.
|
Marwa akijikokota kuinuka baada ya kukalishwa chini na Mchumia Tumbo |
|
Mchumia Tumbo akimuadhibu Marwa |
|
Marwa pu! chini... |
|
Mchumia Tumbo amemkalisha chini Marwa |
|
Marwa na Mchumia Tumbo |
Baada ya pambano, Maneno alikiri kupoteza, lakini akasema amemuonyesha Kaseba kwamba yeye ni nani. “Sikujiandaa vizuri kwa hili pambano, lakini nimetumia akili sana na nimeweza kumaliza raundi zote bila hata kuchuchumaa chini, hii ni kuonyesha kwamba mimi ni bora na niko tayari kurudiana na Kaseba,”alisema.
Kwa upande wake, Kaseba pamoja na kufurahia ushindi alilalamika mpinzani wake kumkumbatia mara kwa mara kumpungua kasi, vinginevyo angemmaliza mapema. “Alikuwa ananikumbatia mikono kila nilipokuwa namemuelemea, ile ilikuwa inanipunguza kasi na hicho ndicho kilichomsaidia,” alisema Kaseba.
|
Mchumia Tumbo kushoto akimuadhibu Marwa |
|
Marwa kushoto amemtupia konde Mchumia Tumbo |
|
Vimwana 'shombe shombe' wakifuatilia mapambano ya ndondi |
|
Konde la Marwa kushoto limepotea njia |