// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); LIGI KUU ZANZIBAR ISITOE MCHEZAJI TAIFA STARS, BASI HATA BENCHI LA UFUNDI? - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE LIGI KUU ZANZIBAR ISITOE MCHEZAJI TAIFA STARS, BASI HATA BENCHI LA UFUNDI? - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Sunday, March 17, 2013

    LIGI KUU ZANZIBAR ISITOE MCHEZAJI TAIFA STARS, BASI HATA BENCHI LA UFUNDI?


    KWA miaka mingi sasa, Zanzibar imepoteza hadhi yake kisoka hasa linapokuja suala la kuchagua wachezaji wa kuichezea timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.
    Imekuwa nadra sana, kwa makocha wanaoajiriwa kuifundisha timu hiyo, kuitupia macho ligi kuu au za madaraja mengine hapa Zanzibar kwa ajili ya kutafuta wachezaji wenye uwezo wa kuwa miongoni mwa nyota wanaounda kikosi hicho.
    Hata pale makocha hao, kuanzia Marcio Maximo hadi Kim Poulsen wa sasa, wanapopata nafasi ya kufanya ziara hapa visiwani kuangalia ligi zetu, hatujawahi kuona wakiwaita wachezaji wanaocheza ligi za hapa ingawa mara kadhaa wamekuwa wakisifu kwamba Zanzibar kuna vipaji.
    Kwangu mimi, sifa hizo zinazotolewa na makocha hao wanapokuja hapa, naziona kama kejeli kwani, kama kweli wameviona vipaji hivyo, sioni sababu ya kutokuita angalau wanasoka wawili kwenye kikosi cha Taifa Stars, timu ya Muungano wa Jamhuri ya Tanzania.
    Imekuwa vigumu kwa wachezaji wanaochezea ligi hapa nyumbani, kupata nafasi ya kuteuliwa katika timu ya Taifa, hadi pale wanaposajiliwa na klabu za Tanzania Bara.
    Siwezi kufahamu kwa uhakika sababu ya hali hii, kwani kama hoja ni ligi ya Zanzibar kutokuwa na mvuto na ushindani, sababu inayoegemewa na wengi, huwa ninajiuliza huwaje macho ya klabu mbalimbali zivione vipaji hivyo na kuwatupia ndoana wanandinga hao?
    Si kweli kwamba klabu za Yanga, Simba, Azam, JKT Oljoro, Mtibwa Sugar na nyengine zenye wachezaji kutoka Zanzibar, wamewaona kwenye mashindano ya kimataifa yakiwemo Chalenji au Kombe la Kagame, kwani si wote wanaosajiliwa huko wamewahi kushiriki mashindano hayo iwe na timu ya taifa, Zanzibar Herioes, au klabu zao.
    Hii inaonesha kuwa, klabu hizo zinafanya kazi kwa kuwatuma watu wao kutafuta vipaji hapa nchini kupitia ligi za madaraja mbalimbali, na ndio maana zinaviona na kuvivuta katika klabu zao.
    Sasa, kama klabu zinaweza kuhangaika na kuvigundua vipaji vilivyoshehni hapa Zanzibar, iweje Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linashindwa kuonesha wajibu wake juu ya timu ya taifa, kwa kuwasaka wanasoka wa Zanzibar kwa kuwapa nafasi makocha, ili wachague wale wanaohisi wanafaa?
    Kwani mchezaji mpaka asajiliwe na Yanga, Simba au Azam ndipo kipaji chake kiweze kuonekana?
    Ni ukweli usiofichika kwamba wachezaji wa Zanzibar waliochaguliwa kuchezea Taifa Stars baada ya kuvutwa na klabu hizo kubwa za Bara, walionekana na klabu hizo tangu wakichezea ligi kuu ya Zanzibar au za madaraja mengine.
    Kwa muktadha huo, hata kama inasemwa kuwa ligi kuu ya Zanzibar haina mvuto au ushindani unaoweza kuvidhihirisha vipaji vya wachezaji wazuri, lakini wachezaji hao wapo, na mtu anahitaji jicho la kitaalamu kuweza kuvibaini, jambo ambalo ndilo linalofanywa na klabu zinazowaona na kuwasajili.
    Kama ni vipaji, Zanzibar tunavyo vinavyotumika hapa nchini na nje.
    Mimi hushangaa ninapowaona makocha wa Taifa Stars kwa msaada wa TFF wanafuatilia sana ligi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili kufahamu maendeleo ya wachezaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu, lakini wanashindwa kufuatilia maendeleo ya Ali Badru, Mzanzibari anayechezea klabu ya Al Canal nchini Misri iliyoko ligi kuu.
    Samatta na Ulimwengu, mara nyengine bila kufahamika kama wameshuka viwango, huletwa nchini kwa gharama kubwa kujiunga na Taifa Stars, lakini hilo halifanyiki kwa Ali Badru, ambaye tangu ahamie Misri, taarifa zinasema amekuwa mfungaji mzuri na chachu ya ushindi kwa timu yake.
    Je, ligi kuu ya Tanzania Bara au ya DRC ndivyo vigezo vinavyotakiwa na makocha wa Taifa Stars, kujua mchezaji gani anafaa kuchaguliwa kuchezea timu hiyo?
    Kama ligi yetu ya Zanzibar haiwezi kuzalisha wachezaji wazuri, je, mbona hao hao wamesajiliwa na klabu kubwa za Bara na wakawa lulu hata katika timu ya Taifa?
    Wachezaji hao wamekuzwa na klabu za Bara? Hapana, tunao walimu wengi wazuri hapa Zanzibar katika ngazi ya Central, ambao walifanya kazi kubwa kuwalea na kuwaendeleza wachezaji hao ambao leo, Simba, Yanga na Azam zimeona umuhimu wao na baadae wakaonekana na makocha wa Taifa Stars.
    Sasa kama Zanzibar ina hazina ya vipaji vilivyosheheni kila wilaya mijini na vijijini, kuna haja gani ya kusubiri mpaka wachezaji wetu wasajliwe na klabu za Bara ndipo uzuri wao uonekane?
    Ina maana kwa wale ambao maisha yao hawatapata bahati ya kuvuka maji na kucheza ligi kuu Tanzania  Bara, waishie hapa hapa tu hata kama wana uwezo sawa na wenzao au kuwazidi?
    Ni hivi majuzi tu, kocha mkuu wa Taifa Stars Kim Poulsen, ametangaza kikosi cha wanandinga 23, kwa ajili ya kupambana na Morocco katika mchezo wa kundi C la kanda ya Afrika kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014, zitakazofanyika nchini Brazil.
    Kama ilivyotarajiwa na wengi, kocha huyo ameendeleza mtindo wa kuteua wachezaji wa Zanzibar wanaocheza ligi kuu Tanzania Bara pekee, ingawa katika kikosi chake ameita sura kadhaa mpya, ambapo nadhani wengine angeweza kuwapata kutokana na ligi kuu ya Zanzibar inayoendelea sasa.
    Ingawa miezi kadhaa nyuma wakati wa michuano ya Kombe la Mapinduzi, Poulsen alikuja Zanzibar, na kusifu vipaji vya wachezaji wetu, huku akisema kuwa amewaona baadhi wanaoweza kuchezea Stars, na kuahidi kuwa atawateua. 
    Katika kikosi hicho kinachoingia kambini kesho jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mechi ya dhidi ya Morocco, sura zilezile za wanasoka wa Zanzibar zimeendelea kupata nafasi ingawa wapo wengine kadhaa waliong’ara na wenzao hao nchini Uganda katika mashindano ya Chalenji na kutwaa ushindi wa tatu kwa kuifunga Kilimanjaro Stars.
    Lakini kama hilo haliotshi, jengine ambalo ninaliona linainyima Zanzibar haki yake ya kutoa mchango katika timu ya Taifa ya Tanzania, ni kukosekana kwa watu wake kwenye benchi la ufundi kwa miaka sasa.
    Kuondoka kwa Marcio Maximo katikati ya mwaka 2010 baada ya kumaliza  mkataba wake,  ilikuwa njia ya kumng’oa pia Ali Bushiri aliyekuwa msaidizi wake na pia kocha wa makipa, pamoja na daktari Abdalla Said ‘Kuku’ ambaye aliwahi kuitumikia  Stars.
    Ukiondoa kocha mkuu, kati ya nafasi nyengine za benchi la ufundi, hakuna yoyote inayofaa kupewa mtu kutoka Zanzibar?
    Katika benchi hilo kuna nafasi za kocha msaidizi, kocha wa makipa, meneja, daktari wa timu, mtaalamu wa tibamaungo na mtunza vifaa, zote zimekumbatiwa na wenzetu hao bila kuidhukuru Zanzibar japo nafasi ya ‘mfua jezi’ ili nayo itoe mchango wake katika timu hiyo inayoitwa ya Muungano wa Tanzania.
    Kwa mambo haya na mengine, ndipo wadau wanapokuwa na haki ya kuisukuma Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, ifufue upya jitihada zake za kuiombea Zanzibar uanachama wa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: LIGI KUU ZANZIBAR ISITOE MCHEZAJI TAIFA STARS, BASI HATA BENCHI LA UFUNDI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top