Wachezaji wa JKT Oljoro |
Na Prince Akbar
LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inatarajiwa kuendelea leo kwa Polisi Morogoro kuikaribisha Oljoro JKT ya Arusha kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Hata hivyo, timu hizo haziko katika kinyang’anyiro cha kuwania ubingwa ambapo Yanga ndiyo inayoongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 42 wakati Oljoro JKT inayofunzwa na Alex Mwamgaya ikiwa nazo 21 na Polisi Morogoro pointi 15.
Oljoro JKT iko katika nafasi ya tisa. Polisi Morogoro ambayo katika mzunguko wa pili imebadilika ikiwa chini ya Kocha Adolf Rishard inashika nafasi ya 12 ikiziacha mkiani Toto Africans yenye pointi 14 na African Lyon ambayo ina pointi 13.
Ligi hiyo itaendelea Jumatano (Machi 6 mwaka huu) kwa mechi kati ya Oljoro JKT vs Tanzania Prisons (Sheikh Kaluta Amri Abeid), African Lyon vs Ruvu Shooting (Azam Complex, Chamazi) na Mgambo Shooting vs Mtibwa Sugar (Mkwakwani) wakati Machi 7 mwaka huu ni JKT Ruvu vs Kagera Sugar (Azam Complex, Chamazi).
Machi 9, mwaka huu kutakuwa na mechi mbili; Yanga vs Toto Africans Uwanja wa Taifa), na Azam vs Polisi Morogoro (Azam Complex, Chamazi).
Wakati huo huo: Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, nayo inatarajiwa kuendelea leo katika makundi yote matatu. Villa Squad itaivaa Ashanti United kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam katika moja ya mechi za kundi B.
Kundi A ni mechi kati ya Kurugenzi ya Mafinga dhidi ya Mbeya City wakati Polisi Iringa vs JKT Mlale, na Majimaji vs Mkamba Rangers zilizokuwa zicheze kesho (Machi 2 mwaka huu), sasa zitaumana Machi 3 mwaka huu mjini Iringa na mjini Songea.
Pia kundi B kesho (Machi 2 mwaka huu) ni Green Warriors vs Transit Camp (Mlandizi) wakati keshokutwa (Machi 3 mwaka huu) Polisi Dar vs Tessema (Karume) na Ndanda vs Moro United katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
Mechi za kundi C kesho ni JKT Kanembwa vs Polisi Tabora (Lake Tanganyika), Polisi Mara vs Polisi Dodoma (Karume, Musoma), Morani vs Pamba (Kiteto) na Mwadui vs Rhino Rangers (Kambarage, Shinyanga).