Ofisa Mtendaji Mkuu wa New Habari, Hussein Bashe akimjulia hali Kibanda Mhimbili leo kabla ya kupelekwa Afrika Kusini. |
Na Waandishi Wetu
MHARIRI Mtendaji wa Kampuni ya New Habari 2006, Absalom Kibanda, amesafirishwa kwenda Afrika Kusini jioni ya leo kwa matibabu zaidi, baada ya jana kuvamiwa na watu wasiojulikana.
Tukio hilo la kinyama, linafananishwa na lile alilofanyiwa Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Steven Ulimboka, mwaka jana ambako leo Jeshi la Polisi pamoja na kuunda Jopo la Upelelezi limeshindwa kutoa matokeo ya upelelezi wake.
Kibanda akiwa Muhimbili leo |
Watu watatu waliokuwa na silaha walivamia gari lake na kumtoa nje kisha kuanza kumpiga katika sehemu mbalimbali za mwili wake huku wakimchoma na kitu kikali kwenye jicho lake la upande wa kushoto, kumkata kidole cha upande huo huo na kumng’oa meno mawili, kabla ya kumtekelekeza kwenye eneo la tukio bila kuchukua kitu chochote.
Kibanda akipakizwa kwenye ndege tayari kwa safari ya Afrika Kusini |
Hata hivyo, alisema pamoja na jitihada za madaktari wa Hospitari ya Muhimbili bado wameshauriwa kumpeleka Afrika Kusini kwa ajili ya uchunguzi zaidi katika jicho lake ambalo linaonekana kupata athari zaidi kuliko sehemu yeyote ya mwili wake.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Theophili Makunga, amesema tukio hilo limefanywa na watu waoga ambao wanadhani kwa kufanya hivyo wataweza kuwanyamazisha Waandishi.
Alisema tukio hilo halihusiani na ujambazi, kama wangekuwa majambazi wangeweza kupora vitu kama kompyuta, simu na fedha alivyokuwa navyo katika gari, bali tukio hilo limetokea kwa ajili ya kazi yake.
Makunga alisema Jukwaa litafanya uchunguzi wa kina ili kubaini matukio mbalimbali ya kushambuliwa kwa Waandishi wa Habari yanayoshika kasi nchini.
“Nawaomba Waandishi tuwe na moyo wa subira wakati uchunguzi wa kutekwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wetu wa Jukwaa la Wahariri ukiendelea, ukweli utajulikana”alisema Makunga.
Aidha, kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe alikuwa miongoni mwa viongozi waliofika kumjulia hali Kibanda na baadaye kuzungumza na Waandishi wa Habari juu ya tukio hilo.
Mbowe alisema tukio hilo ni la kiharamia na vyombo vya dola vinatakiwa kuchukua hatua za haraka, ili kulinda uhuru wa Habari na Wana Habari nchini huku akisisitiza umoja na mshikamano kwa kipindi chote.
“Tunaiomba Serikali kuchunguza kwa kina suala hili la Kibanda, kwani ni la kiharamia na si mara ya kwanza kwa watu kufanyiwa kama hivi hapa nchini,” alisema Mbowe.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP na Mwenyekiti wa Chama Cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (MOAT), Reginald Mengi alifika hospitalini hapo kumpa pole Kibanda.
“Tukio hilio ni kubwa na kwa sasa MOAT, tunataka kuhakikisha tunaokoa maisha ya mwenzetu na baadaye tutakaa kuona cha kufanya,”alisema Mengi.