WENGI wameisikia hotuba fupi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete wakati akizindua Uwanja wa Azam Complex wa klabu ya Azam FC wiki hii.
Na Bin Zubeiry |
Kikwete aliyeziponda Simba na Yanga, klabu kongwe nchini kwamba zimebakia na Baraka ya mashabiki wengi, lakini wamedumaa kimaendeleo, alisema; “Mkikubali tu kuwa kivuli na kuruhusu kufanya kama zinavyofanya klabu kongwe, basi mtakuwa mmepotea, waacheni wafanye wenyewe, nyinyi chezeni mpira,”.
Kikwete aliisifu Azam imevunja ukiritimba wa Simba na Yanga katika soka ya Tanzania.
“Klabu kubwa zimebaki na baraka ya kuwa mashabiki wengi tu, ila hawana kitu, maana baada ya kuwekeza kiufundi wao wanawekeza kwenye kamati ya ufundi, matokeo yake wanashinda mechi za hapa hapa Tanzania tu,”alisema.
Rais huyo aliyeongozana na Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Said Meckysadick na viongozi wengine mbalimbali wa Serikali, pia aliipongeza klabu hiyo kwa kuiwakilisha vyema Tanzania kwenye michuano ya Afrika.
“Simba na Yanga ni wa hapa hapa tu, huku wengine wanasajili kwa kukomoana, ila Azam mmeleta mfano kwa Watanzania,”alisema.
Kikwete aliifananisha Azam na klabu ya Barcelona ya Hispania kwa kuwekeza katika soka ya vijana na baadaye kuwauza kwa gharama kubwa.
“Azam inaweza kuwa kama Barcelona kwa kuwazalisha akina Messi, kwani wana mtindo wa Ulaya, kwa kuwa hawaendeshi timu kwa kutumia wanachama,”alisema.
Kikwete aliyeahidi kuongea na wahusika wanaokata kodi ndani ya klabu hiyo ili kuwafanyie ahueni katika mradi huo, alisema kuwa kama soka inachezwa kwa uchawi basi Afrika ingechukua Kombe la dunia mashindano hayo yanapowadia.
Azam FC ilianzishwa na kikundi cha wafanyakazi wa kampuni ya Mzizima Flour Mill, kampuni tanzu ya Bakhresa, makao yake makuu yakiwa Barabara ya Nyerere, Dar es Salaam, lengo la wafanyakazi hao wa kampuni inayomilikiwa na Said Salim Bakhresa, awali ilikuwa ni kucheza kwa ajili ya kujiburudisha, baada ya kazi.
Lakini baada ya kuona wana timu nzuri, Oktoba 16, mwaka 2004, wafanyakazi hao waliisajili rasmi kwa ajili ya kushiriki Ligi Daraja la Nne, wakitumia jina la Mzizima FC.
Ilikuwa wanapokwenda kucheza mechi, wanapitisha michango kiwandani kwa wafanyakazi na mabosi, wanakwenda kucheza.
Baada ya Mkurugenzi Mkuu wa makampuni ya S.S. Bakhresa, Abubakar Bakhresa, aliona ni vyema timu hiyo ihusishe wafanyakazi wa kampuni zote za Bakhresa, na kutumia jina la moja ya bidhaa zao kubwa, Azam.
Kampuni nyingine za Bakhresa ni Food Products Ltd, Azam Bakeries Ltd, Omar Packaging Industries Ltd na kadhalika.
Wazo lake lilikubaliwa na wafanyakazi wa kampuni hiyo, ndipo timu hiyo ikaanza kuitwa Azam SC, badala ya Mzizima. Lakini baadaye Juni 11, mwaka 2007, ilibadilishwa jina tena na kuwa Azam FC.
Azam ilikwenda kwa kasi nzuri kuanzia Daraja la Nne na hadi mwaka 2008, ilifanikiwa kucheza Ligi Kuu, ikipandishwa na makocha King, aliyekuwa akisaidiwa na Habib Kondo. Baada ya kupanda, Azam ilimuajiri kocha wa zamani wa Simba SC, Mbrazil Neider dos Santos, aliyekuwa akisaidiwa na Sylvester Marsh na Juma Pondamali upande wa kuwanoa makipa.
Baadaye ilimuongeza kocha wa viungo, Itamar Amorin kutoka Brazil pia, ambaye awali ya hapo alikuwa msaidizi wa Marcio Maximo katika timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Amorin baaaye akawa kocha Mkuu Azam FC baada ya kufukuzwa Marcus Tinocco. Amorin naye aliondoka ndipo akaja kocha wa sasa, Muingereza Stewart Hall. Hall alifukuzwa Agosti mwaka jana akaajiriwa Mserbia, Boris Bunjak ambaye alifukuzwa Oktoba mwaka jana na kurejeshwa Hall.
Hadi sasa Azam ina mataji matatu katika kabati lake, mawili ya Kombe la Mapinduzi na moja la Kombe la Hisani walilotwaa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mwishoni mwa mwaka jana.
Ikiwa inashiriki michuano ya Afrika kwa mara ya kwanza mwaka huu, Azam FC imeonyesha dalili za kufika mbali kwenye Kombe la Shirikisho baada ya kufika Raundi ya Pili na kuanza vyema katika mchezo wa kwanza, ikishinda ugenini 2-1 dhidi ya Barack Young Controllers II nchini Liberia.
Katika Raundi ya Kwanza, Azam FC iliitoa Al Nasr Juba ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 8-1, ikiifunga 3-1 Dar es Salaam na 5-0 Sudan Kusini.
Azam sasa inahitaji sare katika mchezo wa marudiano na B.Y.C. wiki ijayo ili kusonga mbele. Simba na Yanga zipo tangu miaka ya 1930, lakini zaidi ya majengo yake waliyojenga kwa msaada wa rais wa zamani wa Zanzibar, Hayati Abeid Amaan Karume na kutawala soka ya Tanzania, hazina cha kujivunia- sana baraka ya mashabiki kama alivyosema rais JK.
Kwa kweli hotuba ya JK, japo ilikuwa fupi, lakini ilikuwa nzuri na ina maeneo mengi ya kujadili. Leo, ningependa kujadili eneo moja, Azam isikubali kuwa kivuli cha klabu moja kati ya mbili kongwe nchini, Simba na Yanga.
Bodi ya Ukurugenzi ya Azam inapaswa kutambua, Rais JK aliwapa ujumbe mzito sana hapa. Wapo wafanyabiashara wengine walianzisha timu kabla ya Alhaj Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake, lakini zilikufa kwa sababu zilikubali kuwa kivuli cha klabu moja kati ya mbili kongwe.
Mfano ni Merey Balhboub na Moro United yake. Alianza vyema, lakini alipojiruhusu kuwa kivuli cha Simba SC akaisha. Juma Kaseja ni kipa ambaye aliibukia Moro United mwaka 2001, wengi walimtabiria huyo atakuwa Tanzania One wa baadaye.
Merey hakuona kama kipa huyo ataifaa Moro United bali Simba SC, akampa fedha Sh. Milioni 2 wakati huo na gari aina ya Toyota Mark II aje Dar es Salaam kuchezea Simba SC.
Nimetoa mfano wa Kaseja, kwa sababu huyo ndiye ambaye amefanikiwa na amedumu katika soka ya Tanzania, lakini Merey aliwatoa wachezaji wengi wazuri wa Moro United kuwapeleka Simba kama Shengo Tondola, Abuu Amrani na wengineo.
Alifanya hivyo kwa mapenzi yake tu kwa Simba SC akaigeuza Moro United kuwa kivuli cha Simba na matokeo yake, japo bado ipo lakini timu hiyo kwa miaka saba sasa haipo katika miliki yake na msimu huu imeshuka hadi Ligi ya Mkoa.
Hata Mohamed Dewji alipoinunuaa African Lyon, alikuwa ana mipango mizuri sana, lakini hakufika mbali kwa sababu kulikuwa kuna dalili za kuifanya timu hiyo kuwa kivuli cha Simba SC.
Toto African ya Mwanza ile, ni kivuli cha Yanga inanufaika na nini? Mbona ina bahati ya kupata vipaji vizuri sana na inavitumiaje kujinufaisha? Toto ni miongoni mwa timu zinazotoa wachezaji wengi kuja timu kubwa, Simba, Yanga na Azam yenyewe- inanufaika na nini?
Kama Toto inaweza kuwa timu yenye kuaminika kuwa na uwezo wa kuifunga Simba SC, basi inaweza kuifunga timu nyingine yoyote ikiwemo hiyo ya Yanga, lakini kwa kuwa imekubali kuwa kivuli, imekwisha.
Azam, wanajua uhusiano wao na Simba SC ambao tayari wapinzani wao wa jadi, Yanga SC wameanza kuutilia shaka hivyo basi, warejee kauli yake Rais JK na kujitazama mara mbili, ili waepuke kuwa kivuli. Zaidi ya hayo, naungana na JK kuipongeza Azam na kuwatakia mafanikio zaidi.