Naibu Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Amosi Makala akimkabidhi kombe la Ubingwa wa michuano ya NSSF Media Cup 2013 kwa naodha wa timu ya Jambo Leo, Said Mwishehe katika baada ya kuifunga Changamoto bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliofanyika leo kwenye Uwanja wa TCC Chang’ombe jijini Dar es Salaam. (Picha na Habari Mseto Blog)
Naibu Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Amosi Makala akimkabidhi kombe la Ubingwa wa michuano ya NSSF Media Cup 2013 kwa naodha wa timu ya Business Times Queens, Lulu Habibu baada ya kuifunga TBC 39-18 katika mchezo wa fainali uliofanyika leo kwenye Uwanja wa TCC Chang’ombe jijini Dar es Salaam.Na Mwandishi Wetu
TIMU za Jambo Leo na Business Times (BTL), leo zimefanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano ya NSSF Media Cup 2013, baada ya kushinda mechi zao za fainali ya soka na netiboli dhidi ya Changamoto na TBC.
Katika fainali ya soka, bao pekee la kipindi cha kwanza la mshambuliaji Julius Kihampa, lilitosha kuwapa Jambo Leo ubingwa wa pili wa michuano hiyo iliyofanyika kwa mwaka wa 10 na harakati za Changamoto kusawazisha hazikuzaa matunda.
Kwa upande wa Netiboli, Business Times Queens ‘The Bize,’ ilifanikiwa kutwaa ubingwa wa mchezo huo kwa ushindi wa magoli 39-18 dhidi ya TBC, huku nyota wake Lulu Habibu akifunga mara 27.
Lulu alitwaa tuzo ya mfungaji bora wa michuano hiyo upande wa netiboli kwa kufikisha magoli 153 katika mechi nne alizocheza, huku tuzo hiyo kwa upande wa soka ikitwaliwa na Nurdin Msindo wa Tumaini Media, aliyefunga mabao manne.
Lulu na Nurdin kila mmoja alizawadiwa kiasi cha shilingi 300,000 ambayo ni zawadi kwa wafungaji bora, huku Sahara Media ikitwaa tuzo ya timu yenye nidhamu, ambapo walizawadiwa kikombe.
Kwa kutwaa ubingwa soka, Jambo Leo walizawadiwa kikombe na shilingi mil. 4, huku Changamoto wakitwaa shilingi mil. 3 kwa kushika nafasi ya pili na TBC wakizoa shilingi mil. 2 kwa kutwaa nafasi ya tatu - baada ya juzi Ijumaa kuwalaza IPP kwa penati 4-3.
‘The Bize Queens’, wamebeba kombe na shilingi mil. 3.5 za ubingwa wa netiboli, huku mshindi wa pili TBC wakilamba shilingi mil. 2 na mshindi wa tatu NSSF wakibeba kombe pekee na kitita chao cha shilingi mil. 1 wakikitoa kwa Tumaini iliyoshika nafasi ya nne.
NSSF Media Cup 2013 ni michuano iliyofanyika kwa wiki mbili kwenye viwanja vya TCC na DUCE vilivyoko Chang’ombe jijini Dar es Salaam, ikihusisha timu 17 za soka na 15 za netiboli zilizoundwa na wafanyakazi wa vyombo vya habari nchini.
Baada ya michuano hiyo kuzinduliwa na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaundencia Kabaka Machi 9, ilihitimishwa leo kwa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Amos Makalla kukabidhi zawadi kwa washindi wapya.