VIONGOZI wa TFF. Viongozi wa vyama vya soka vya mikoa. Wageni waalikwa. Waandishi wa Habari, Mabini na Mabwana;
Nafurahi kujumuika nanyi hapa leo nikiwakilisha kampuni ya Coca-Cola, ambao ndio wadhamini wa mashindano ya soka ya vijana ya Copa Coca-Cola.
§ Mabibi na Mabwana, Coca-Cola tunajivunia mafanikio ya Copa Coca-Cola hapa Tanzania ambayo yamepatikana kwa kipindi cha miaka sita ya ushirikiano wetu na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
§ Mtakubaliana na mimi kwamba michuano ya Copa Coca-Cola imekuwa ndio chimbuko kubwa la wachezaji wa soka hapa Tanzania, kuanzia kwenye Ligi ya Daraja la Kwanza, Ligi Kuu, timu za taifa za vijana na hata timu ya wakubwa ya Taifa yaani Taifa Stars.
§ Napenda kutoa shukrani za dhati kwenu nyinyi viongozi wa vyama vya soka vya mikoa kwa kusimamia na kuhakikisha kwamba michuano ya Copa Coca-Cola inafanyika vizuri kila mwaka kwenye mikoa yenu. Kujitolea kwenu kumeiwezesha michuano hii kuwa nguzo muhimu kwenye maendeleo ya soka hapa Tanzania.
§ Wakati mkishiriki semina hii, napenda kuwahakikishia kwamba kampuni ya Coca-Cola ina nia thabiti ya kuendelea kuunga mkono michuano hii ambayo haichezwi hapa Tanzania tu bali katika sehemu nyingine duniani. Lengo letu ni kutumia mashindano haya kama chombo cha kuibua vipaji vya soka na kuwafanya vijana kuwa wachangamfu na wenye afya nzuri. Pia tunafahamu kwamba katika dunia ya leo mchezo wa soka ni chanzo cha ajira kwa vijana wengi.
§ Mabibi na Mabwana, kuanzia mwaka huu wa 2013, Copa Coca-Cola inabadilika kuwa michuano ya vijana wenye umri chini ya miaka 15, kutoka kuwa miaka 17 ya hapo awali. Sababu ya mabadiliko hayo ni kwamba tunataka kufikia vijana wengi zaidi kama ilivyoelekezwa na Shirikisho la Soka duniani (FIFA). Pia, michuano hii sasa itakuwa inaanza Aprili na kumalizika Septemba.
§ Taratibu zingine za michuano hii zinabakia kama kawaida kwa ni michuano ya kila mwaka kuanzia ngazi ya wilaya hadi Taifa ikishirikisha Tanzania Bara na Zanzibar.
§ Ni imani yetu kuwa michuano ya Copa Coca-Cola pamoja na michezo mingine ambayo tunathamini kama Sprite Slam Basketball, itaendelea kuwa chachu kwa vijana wa Kitanzania na kuwafanya kung’ara katika medani ya kimataifa. Kwa miaka sita iliyopita, tumeweza kushuhudia timu za Copa Coca-Cola zikifanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa nchini Brazil mwaka wa 2007 na 2008 na Afrika Kusini 2009/2010/2011/2012.
§ Mbali na kupata fursa ya kuonekana kimataifa, michuano ya Copa Coca-Cola inatoa zawadi mbali mbali kwa mchezaji mmoja mmoja na kwa timu. Timu tatu bora hupata medali, vyeti na fedha taslimu. Wengine ni mchezaji bora, mfugaji bora, golikipa bora, mwamuzi bora na timu yenye nidhamu.
§ Copa Coca-Cola ilizinduliwa hapa Tanzania 2007. Hata hivyo, udhamini wa Coca-Cola kwenye soka na michezo kwa ujumla ulianza tangu 1928 kwa kudhamini Olimpiki na soka 1930. Coca-Cola imekuwa ikishirikiana na FIFA tangu 1974 na imekuwa mdhamini rasmi wa Kombe la Dunia tangu 1978.
§ Kwa kumalizia, napenda kushukuru kila mmoja wenu kwa kuweza kuja kujumuika nasi katika semina hii na naomba tuendelee na moyo huo kwa ajili ya kuendeleza soka hapa nchini,
Asanteni.