Mabalozi shujaa; Wachezaji wa Azam FC |
Na Mahmoud Zubeiry
WAWAKILISHI pekee wa Tanzania waliobaki katika michuano ya Afrika, Azam FC ya Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam jana wamejiweka katika nafasi nzuri ya kuingia Raundi ya Tatu ya Kombe la Shirikisho Afrika, kufuatia ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya wenyeji Barrack Young Controllers katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Pili uliofanyika kwenye Uwanja wa Antonette Tubman Monrovia, Liberia.
Kwa matokeo hayo, Azam sasa itahitaji hata sare tu ili kusonga mbele, Raundi ya Tatu na ya mwisho ya mchujo kabla ya hatua ya makundi.
Shujaa wa Azam FC jana alikuwa ni Seif Abdallah Karihe aliyefunga bao la ushindi dakika ya 90, zikiwa ni dakika 10 tangu aingie uwanjani kuchukua nafasi ya Kipre Tchetche, kufuatia kazi nzuri ya Mzanzibari mwenzake, Khamis Mcha ‘Vialli’.
Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Farouk Mohamed kutoka Misri, hadi mapumzikko, B.Y.C. walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililofungwa na Junior Barshall dakika ya 44 na Azam wangeweza kuondoka uwanjani baada ya dakika 45 za kipindi cha kwanza wakiwa wana mabao, iwapo wangetumia vizuri nafasi nzuri takriban sita walizopata.
Kwa muda mrefu kipindi cha kwanza, B.Y.C. walikuwa wanacheza kwa kujihami zaidi wakiwategeshea mitego ya kuotea wachezaji wa Azam FC na kipindi cha pili Azam FC baada ya kupata mawaidha ya kocha wao, Muingereza Stewart Hall walirejea uwanjani wamebadilika na kufanikiwa kusawazisha bao.
Alikuwa ni kiungo wa kimataifa wa Kenya, Humphrey Mieno aliyeifungia bao la kusawazisha Azam FC na sasa Azam inatarajiwa kurejea nchini kesho na mchezo wa marudiano utafanyika wiki mbili zijazo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, kikosi cha Azam FC kilikuwa; Mwadini Ally, Himid Mao, Waziri Salum, David Mwantika, Joackins Atudo, Ibrahim Mwaipopo aliyempisha Abdi Kassim ‘Babbi’ dakika ya 68, Humphrey Mieno, Kipre Balou, Khamis Mcha ‘Vialli’, John Bocco ‘Adebayor’ aliyempisha Jabir Aziz dakika ya 85 na Kipre Tcheche aliyempisha ‘mshindi wa mechi’, Seif Abdallah Karihe dakika ya 80.
Huu ni mwanzo mzuri kwa Azam na pia uthibitisho wa ubora wa timu yao hata kama haitatwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, lakini sasa imani ipo kwamba Watoto hao wa Alhaj Said Salim Awadh Bakhresa watafika mbali katika michuano ya Afrika, tofauti na Simba na Yanga zetu ambazo huchungulia tu na kurudi hapa hapa.
Hizi ni dalili kwamba, kilio cha Watanzania kuona nchi yao inakuwa na timu tishio kama ilivyo TP Mazembe ya DRC sasa kinakaribia kwisha. Azam washindani. Wana mipango. Hii ni timu ambayo ilianza programu ya maandalizi ya mwaka huu, tangu Novemba mwaka jana.
Walianza mazoezi pale kambini kwao Chamazi Novemba na Desemba wakaenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kucheza Kombe la Hisani, ambalo walitwaa. Waliporejea wakaenda kwenye Kombe la Mapinduzi Zanzibar ambako pia walitwaa. Baada ya hapo, wakaenda kucheza mechi tatu za kirafiki Kenya dhidi ya timu bora za huko, na wakafungwa moja, wakashinda mbili.
Usisahau kuhusu usajili makini katika dirisha, kusajiliwa mabeki wawili wa nguvu, David Mwantika kutoka Prisons ya Mbeya na Joackins Atudo wa Kenya, kiungo Humphrey Mieno kutoka Kenya na washambuliaji Brian Umony kutoka Uganda na Seif Abdallah kutoka Ruvu Shooting ya Pwani.
Hawakusajili kwa fasheni kama ambavyo tumezoea wale wanaoitwa vigogo wa soka nchini wanavyosajili- walijua wamefukuza mabeki watatu kwa tuhuma za rushwa, wakiwemo wawili wa kati Said Mourad na Aggrey Morris ukiachilia mbali beki wa pembeni Erasto Nyoni, hivyo wakaleta Atudo na Mwantika. Wale watu wanavyocheza sasa, utafikiri ‘walizaliwa tumbo moja’.
Azam FC kwa sasa ni timu bora na hiyo ni kwa sababu soka haichezwi kizani nasi tunaiona. Nani amesahau jinsi Yanga walivyokuwa wakifanya hila za kupoteza muda kwa kujiangusha angusha ili mchezo uishe walinde ushindi wao wa 1-0 walipocheza na Azam katika Ligi Kuu hivi karibuni?
Lakini pamoja na ukweli huo, Azam FC wanapaswa kujua haya ni mashindano (CAF) na kila timu imeingia huko kupambana. Azam wazingatie kwamba, ushindi wa 2-1 ni katika matokeo ya awali tu ambayo hayahitimishi chochote katika hatua hii.
Azam, wanapaswa kutobweteka na kujiandaa vyema kwa ajili ya mchezo wa marudiano ambao ndio utaamua hatima yao katika mashindano haya. Matumaini yapo, lakini wasibweteke.
Kila siku tunaimba historia ya Simba kufungwa 4-0 Dar es Salaam na Mufulira Wanderers ya Zambia mwaka 1979 nayo ikaenda kulipa kisasi cha kushinda 5-0 ugenini katika Ligi ya Mabingwa, basi Azam wajue hata B.Y.C. inaweza kufanyia kazi mapungufu yake na ikaja kufanya maajabu Dar es Salaam.
Hivyo basi, Bodi ya Ukurugenzi ya Azam FC, Menejimenti, benchi la ufundi na wachezaji wanapaswa kujua, tiketi yao ya kusonga mbele wataipata baada ya dakika 90 za mchezo wa marudiano wiki ijayo. Hongera Azam FC, lakini kazi bado.