Abbel Dhaira; Atabeba Simba leo? |
Na Mahmoud Zubeiry
KIPA Mganda, Abbel Dhaira leo ataanza kwenye lango la Simba SC katika mchezo wa marudiano wa Raundi ya Kwanza, Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji wa Recreativo de Libolo, utakaopigwa kwenye Uwanja wa Manispaa mjini Calulo, Angola.
Akizungumza kwa simu kutoka Calulo, Angola- kocha wa Simba, Mfaransa Patrick Liewig alisema beki wa kulia atakuwa Nassor Massoud ‘Chollo’, kushoto Amir Maftah, wakati katikati watasimama Komabil Keita na Juma Nyosso.
Kocha huyo wa zamani wa akademi ya PSG ya Ufaransa na ASEC Abidjan ya Ivory Coast, alisema safu ya kiungo leo itaundwa na Shomary Kapombe nyuma, Abdallah Seseme mbele, kushoto na kulia Haroun Chanongo na Salim Kinje na washambuliaji Amri Kiemba na Felix Sunzu.
Mwinyi Kazimoto anasumbuliwa na maumivu ya jino bado, ingawa jana alifanya mazoezi kidogo lakini anaanzia benchi jioni hii.
Juma Kaseja yuko fiti kabisa, lakini Liewig amesema Dhaira anaonekana kuwa bora zaidi kuelekea mchezo wa leo, kuliko Simba One huyo.
Ikumbukwe, Simba iliyofungwa 1-0 katika mchezo wa kwanza mjini Dar es Salaam, inahitaji ushindi wa 2-0 ili kusonga mbele.
Kwa upande wake, Mkuu wa Msafara wa Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema hali ya kambi ni nzuri hadi sasa na hakuna tatizo lolote.
“Tumetoka kwenye kikao muda huu, mwalimu amezungumza, nasi viongozi tumetoa nasaha zetu, sasa tunajiandaa kuondoka hapa saa 7:00 (saa 9:00 kwa saa za Afrika Mashariki) kuelekea uwanjani, mechi inaanza saa Saa 9:00 za hapa,”alisema Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
Katika kuwapa motisha wachezaji ili washinde mechi ya leo, Hans Poppe amewaahidi donge nono la Sh. Milioni 10 iwapo watashinda mechi hiyo, ahadi ambayo aliitoa pia kabla ya mechi ya kwanza Dar es Salaam.
KIKOSI; Abbel Dhaira, Nassor Massoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Komabil Keita, Juma Nyosso, Shomary Kapombe, Amri Kiemba, Abdallah Seseme, Haroun Chanongo, Felix Sunzu na Salim Kinje.
BENCHI; Juma Kaseja, Kiggi Makassy, Mwinyi Kazimoto, Mrisho Ngassa, Ramadhani Chombo ‘Redondo’ na Abdallah Juma.