MSHAMBULIAJI wa Galatasaray, Didier Drogba ametemwa katika kikosi chawachezaji 28 cha Ivory Coast kitakachomenyana na Gambia kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 Jumammosi ijayo, jambo mambalo linaashiria mwisho wake katika soka ya kimataifa.
Nyota huyo wa zamani wa Chelsea alikuwa sehemu ya kikosi cha Galatasaray kilichofuzu Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuitoa Schalke kwa jumla ya mabao 4-3 na Nahdha huyo wa Ivory Coast alitarajiwa kujumuishwa kwenye kwenye kikosi cha mechi hiyo ya Kundi C lenye timu za Tanzania na Morocco pia.
Drogba, ambaye ameichezea mechi 95 nchi yake, inafahamika hana uhusiano mzuri na kocha wa sasa wa Tembo wa Ivory Coast, Sabri Lamouchi ambaye aliwahi kumtema kwenye mechi moja wakati wa Fainali za Mataifa ya Afrika hivi karibuni.
Ametemwa: Mshambuliaji huyu hajaitwa kwenye kikosi kitakachoivaa Gambia
Chama cha Soka Ivory Coast bado hakijatoa sababu za kutemwa kwa mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 35, lakini inafikiriwa kilikuwa kinatilia shaka kiwango chake hasa baada ya kutofanya vizuri China alipokuwa akiichezea Shanghai Shenhua na pia kuboronga kwenye Mataifa ya Afrika hivi karibuni Afrika Kusini.
Gwiji huyo wa Stamford Bridge si mkongwe pekee aliyetemwa kwenye kikosi cha Tembo, bali hata beki anayecheza naye Galatasaray, Emmanuel Eboue pia amefungiwa vioo.
Kwa sasa, Ivory Coast inaongoza Kundi C kwa pointi zake nne baada ya mechi mbili na Drogba alitazamiwa kuongoza kampeni za nchi yake kuwania tiketi ya Brazil 2014, ambayo itakuwa mara yake ya mwisho katika majukumu ya kitaifa.