Na Mahmoud Zubeiry
AZAM FC imejiweka sawa katika kuifukuza Yanga SC kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya jioni hii kuilaza mabao 3-0 Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, Azam imefikisha pointi 40 na kubaki inazidiwa pointi nane na Yanga SC.
Tchetche akifunga |
Hadi mapumziko, tayari Azam walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililowekwa nyavuni na mshambuliaji kutoka Ivory Coast, Kipre Herman Tchetche dakika ya 17.
Tchetche alifunga bao zuri, baada ya kupokea pasi ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na kuambaa pembezoni upande wa kushoto mwa Uwanja akiingia ndani, kama anataka kupiga krosi lakini akaunganisha mwenyewe nyavuni kwa shuti kali la kushitukiza.
Azam ingeweza kupata mabao mawili zaidi kipindi cha kwanza kama ingekuwa makini kutumia nafasi ilizozitengeneza.
Prisons walicheza vizuri na walikaribia kufunga mara mbili kwa mashambulizi ya kutokea upande wa kushoto mwa Uwanja.
Kipindi cha pili, Azam walirejea na kasi zaidi na kufanikiwa kupata mabao mawili zaidi, yaliyofungwa na John Raphael Bocco ‘Adebayor’ dakika ya 76 na Tchetche tena dakika ya 84.
Katika mchezo huo, kikosi cha Azam FC kilikuwa; Mwadini Ally, Himid Mao, Waziri Salum, Luckosn Kakolaki, Joackins Atudo, Kipre Balou, Kipre Tchetche, Salum Abubakar/Ibrahim Mwaipopo, John Bocco, Humphrey Mieno/Abdi Kassim ‘Babbi’ na Khamis Mcha ‘Vialli’.
Priosns FC; David Burhan, Aziz Sibo/Henry Mwalugala, Laurian Mpalule, Lugano Mwangama, Jumanne Elfadhil, Nurdin Issa, Jeremiah Mgunda, Khalid Fupi, Elias Maguli, Freddy Chudu/ Peter Kizengele na Ramadhani Katamba/Hamisi Mango.