Azam FC |
Na Princess Asia
AZAM FC, sasa itamenyana na Barrack Young Controllers II ya Liberia, nchi anayotoka mwanasoka pekee wa Afrika kuwahi kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa Ulaya na Dunia, George Opong Weah katika Raundi ya Pili ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika, kufuatia jana kuitoa Al Nasir Juba ya Sudan Kusini.
Azam jana imeitoa Al Nasir, kufuatia ushindi wa ugenini wa mabao 5-0, ambao unafanya ushindi wake wa jumla uwe 8-1, baada ya awali kushinda 3-1 Dar es Salaam.
Barrack Young Controllers II nayo imeifunga Johansens ya Sierra Leon bao 1-0 ugenini kufuatia sare ya bila kufungana katika mchezo wa awali ugenini.
Kama ilivyotarajiwa na wengi, Azam ndio timu pekee iliyobaki kwenye michuano ya Afrika, baada ya jana kuitoa Al Nasir ya Juba.
Katika mchezo huo, mabao ya Azam yalifungwa na Kipre Herman Tchetche, John Raphael Bocco kila mmoja mawili, moja kila kipindi na lingine Khamis Mcha ‘Vialli’.
Jamhuri ya Pemba, ilikuwa timu ya kwanza ya Tanzania kuaga michuano ya Afrika, baada ya jana jioni kufungwa mabao 5-0 na wenyeji Kedus Giorgis nchini Ethiopia katika mchezo wa marudiano, Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika.
Matokeo hayo, yanamaanisha, Jamhuri imeaga kwa kufungwa jumla ya mabao 8-0, baada ya awali kutandikwa 3-0 katika mchezo wa kwanza Uwanja wa Gombani, Pemba.
Wawakilishi wengine wa Bara katika michuano hiyo, Simba SC wametolewa pia baada ya kufungwa mabao 4-0 na Recreativo de Libolo ya Angola kwenye Uwanja wa Manispaa mjini Calulo, Angola.
Matokeo hayo, yanaifanya Simba itolewe kwa jumla ya mabao 5-0, baada ya awali kufungwa bao 1-0 Dar es Salaam.
Azam wataanzia ugenini mechi ya kwanza, kati ya Machi 15 na 17, mwaka huu kabla ya kurudiana wiki mbili baadaye na wakivuka mtihani huo watakutana na mshindi kati ya FAR Rabat ya Morocco na Al Nasr ya Libya.