Wachezaji wa Ashanti wakishangili bao lao la kwanza, leo dhidi ya Villa Squad, Ashanti imerejea Ligi Kuu. |
Na Mahmoud Zubeiry
ASHANTI United ‘Watoto wa Jiji’, wamefanikiwa kurejea Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kufuatia sare ya 2-2 jioni ya leo na Villa Squad ya Kinondoni, katika mchezo wa Kundi B, Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Karume, Ilala mjini Dar es Salaam.
Kwa sare hiyo, wauza mitumba hao wa soko la Ilala, mkabala na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, wamefikisha pointi 28, baada ya kucheza mechi 15, ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote, zikiwa zimebaki mechi mbili mbili.
Villa ndio waliokuwa wapinzani wakuu wa Ashanti katika kundi hilo katika kinyang’anyiro cha kupanda na kwa sare hiyo wanafikisha pointi 20 na hata wakishinda mechi mbili zilizobaki na Ashanti ikafungwa zote, watafikisha pointi 26.
Ulikuwa mchezo mtamu wenye upinzani mkali, ladha zaidi ikiwa ni mizuka ya mashabiki wa timu zote mbili, wale ‘masela’ wa mchangani ambao walifanya vitimbi vya aina yake, ikiwemo kuingia uwanjani na kutisha marefa- matusi ya nguoni ndio usiseme, pole mama zetu, leo wamedhadhalishwa.
Hadi mapumziko, tayari nyavu za kila timu zilikuwa zimekwishatikisika mara moja, Ashanti wakitangulia kupata bao na Villa kukomboa.
Bao la Ashanti lilifungwa na beki wa Villa, Zablon Raymond aliyejifunga dakika ya 10 akitaka kutoa mpira nje, kabla ya Ally Mrisho kuisawazishia Squad dakika ya 30.
Kipindi cha pili kasi ya mchezo iliongezeka na Ashanti walikuwa wa kwanza tena kuwainua mashabiki wao kwa bao la Faki Rashid dakika ya 54, kabla ya Villa kusawazisha tena dakika ya 65 kupitia kwa Amri Mwindeni.
Villa walijitahadi kusaka bao la ushindi, lakini Ashanti walisimama imara kuhakikisha leo wanajihakikishia tiketi ya kurejea Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam tangu washuke mwaka 2008.
Baada ya mechi, mashabiki wa Ashanti walitoka kwa maandamano, wakiwa wamewasha mishumaa na kuimba nyimbo za kuvutia kuelekea mitaa ya Ilala huku wakipuliza vuvuzela zao.