// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); YANGA WALEEEEE, TEGETE KAMA KAWA, NIZAR, KAVUMBANGU WAJIKUMBUSHIA KUFUNGA - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE YANGA WALEEEEE, TEGETE KAMA KAWA, NIZAR, KAVUMBANGU WAJIKUMBUSHIA KUFUNGA - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Wednesday, February 13, 2013

    YANGA WALEEEEE, TEGETE KAMA KAWA, NIZAR, KAVUMBANGU WAJIKUMBUSHIA KUFUNGA

    Simon Msuba kushoto akimpongeza Tegete

    Na Mahmoud Zubeiry
    YANGA SC imejitanua kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kufuatia ushindi wa mabao 4-0 jioni hii dhidi ya African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Matokeo haya, yanaifanya Yanga itimize pointi 36, baada ya kucheza mechi 16, ikiwazidi Azam FC pointi tatu katika nafasi ya pili na mabingwa watetezi, Simba SC wanashika nafasi ya tatu kwa pointi zao 28.
    Hadi mapumziko, Yanga walikuwa tayari wanaongoza kwa mabao 2-0, ambayo yote yalitiwa kimiani na Jerry Tegete.
    Tegete ambaye aliuanza mchezo huo vibaya akikosa mabao mawili ya wazi mwanzoni, kiasi cha mashabiki kuanza kupiga kelele za kutaka atolewe, alirekebisha makosa yake na kuwainua vitini mara mbili mashabiki hao kabla ya filimbi ya kuugawa mchezo.
    Alifunga bao la kwanza dakika ya 21, akiunganisha kwa kichwa krosi maridadi ya winga Simon Msuva, wakati la pili alifunga ‘Kizungu’  kwa kisigino baada Hamisi Kiiza kushindwa kuiunganisha krosi ya Juma Abdul na mpira ukampita na kumkuta mfungaji.
    Kipindi cha pili, Yanga walirudi na moto zaidi, na kufanikiwa kuongeza mabao mawili, huku wakipoteza nafasi ya wazi ya kufunga bao moja zaidi kwa kupoteza penalti.
    Hamisi Kiiza hakuwa mwenye bahati siku ya leo, kwani alikosa penalti dakika ya 47 baada ya kipa Abdul Seif kudaka, kufuatia beki Ibrahim Job kumchezea rafu Haruna Niyonzima kwenye eneo la hatari. 
    Didier Kavumbangu aliyeingia kuchukua nafasi ya Jery Tegete aliifungia Yanga bao la tatu kwa penalti dakika ya 69, baada ya beki Sunday Bakari kuunawa mpira kwenye mpira eneo la hatari.
    Yanga ilihitimisha karamu yake mabao jioni ya leo kupitia kwa kiungo Nizar Khalfan aliyeingia kipindi cha pili pia kuchukua nafasi ya Simon Msuva, aliyefunga bao la nne dakika ya 80 kwa shuti akiunganisha krosi ya Saidi Bahanuzi, aliyetokea benchi pia kumpokea Kiiza.
    Yussuf Mlipli alitolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 90, baada ya kumchezea rafu David Luhende. 
    Refa Martin Saanya wa Morogoro alikimbizwa na wachezaji wa Lyon dakika ya 47 baada ya kuwapa penalti Yanga, na pamoja na wachezaji wengine kuonekana kumsukuma huku akikimbia hadi nje ya Uwanja, lakini alitoa kadi mbili tu na njano kwa Sunday Bakari na Yussuf Mlipili.  
    Wachezaji hao walitulizwa na kocha wa Salim Bausi, ambaye aliingia uwanjani baada ya kuona wanazidi kumtia kashikashi refa. 
    Refa msaidizi namba moja, Omar Kambangwa wa Dar es Salaam, alilazimika kuwaomba radhi wachezaji wa Yanga dakika ya 38 baada ya kumnyooshea kibendera cha kuotea Kiiza akiwa anakwenda kufunga, wakati beki mmoja wa Lyon alikuwa kwenye eneo la lango lao.
    Katika mchezo huo, kikosi cha Yanga kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, David Luhende, Nadir Haroub ‘Canavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva/Nizar, Frank Domayo, Jery Tegete/Kavu, Hamisi Kiiza/Bahanuzi na Haruna Niyonzima.
    African Lyon; Abdul Seif, Yussuf Mlipili, Sunday Bakari, Ibrahim Job, Obina Salamusasa, Abdulghan Gulam, Amani Kyata, Mohamed Samatta, Iddi Mbaga/Mgwao/Jacob masawe, Bright Ike na Adam Kingwande/Benedict Mwamlangala.
    Katika mechi nyingine, Toto African ilitoka 2-2 na Polisi Moro kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza wakati Mtibwa Sugar nayo imelazimishwa sare ya bila kufungana na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.
    Yussuf Mlipili akimkwatua David Luhende

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YANGA WALEEEEE, TEGETE KAMA KAWA, NIZAR, KAVUMBANGU WAJIKUMBUSHIA KUFUNGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top