Kikosi cha Yanga SC |
Na Mahmoud Zubeiry
BAADA ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Kagera Sugar Jumatano, ambao umezidi kuwawekea ‘zege’ kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, vinara wa ligi hiyo, Yanga SC wametoa mapumziko ya siku mbili kwa wachezaji, kesho na keshokutwa kabla ya kuanza tena mazoezi Jumatatu.
Yanga iliitandika Kagera Sugar 1-0, bao pekee la kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima Jumamosi na kufikisha pointi 42, hivyo kujiimarisha kileleni mwa Ligi Kuu, ikiwazidi Azam wanaowafuatia katika nafasi ya pili kwa pointi sita.
Ofisa Habari wa Yanga SC, Baraka Kizuguto ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, timu imefanya mazoezi leo asubuhi na baada ya hapo, wachezaji wamepewa mapumziko hadi Jumatatu.
Kizuguto alisema kwa kuwa mechi ijayo dhidi ya Toto Africans ni wiki ijayo, wanaamini mapumziko hayo ya wikiendi hayataiathiri timu kwa namna yoyote.
“Tutakuwa na muda wa siku tano kuanzia Jumatatu kujiandaa na mechi na Toto, zitatosha sana, na wachezaji wanajua umuhimu wa kutwaa ubingwa, hivyo tunaamini hawatayatumia vibaya mapumziko haya,”alisema Kizuguto.
Yanga inaendelea vizuri na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ikiwa na pointi 42 baada ya kucheza mechi 18, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 36, wakati mabingwa watetezi Simba SC, wenye pointi 31, wanashika nafasi ya tatu.