Pierre Wome |
Na Mahmoud Zubeiry
BEKI wa kimataifa wa Cameroon, Pierre Nlend Wome na Nahodha wa kikosi cha timu hiyo katika mchezo wa leo, dhidi ya Tanzania, amesema kwamba wachezaji wa Afrika wanatakiwa kuongeza juhudi ili kupata mafanikio kama waliyopata wachezaji waliowatangulia.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, Wome aliyezaliwa Machi 26, mwaka 1979 mjini Douala, Cameroon, ambaye kwa sasa anachezea Coton Sport FC de Garoua ya nyumbani kwao, amesema kwamba idadi ya wachezaji wa Afrika wanaotamba katika ulimwengu wa soka inaenda ikipungua.
Akitolea mfano Cameroon, alisema kuna wakati ilikuwa ina wachezaji wengi katika klabu kubwa Ulaya, lakini kwa sasa wamefutika na hiyo inatokana na soko yao kushuka.
"England kuna wakati Wacameroon walikuwa wanafanya vizuri sana pale, Eric Djemba Djemba alikuwa Manchester United, Rigobert Song alikuwa Liverpool, Marc Vivien Foe alikuwa Manchester City na mimi nilikuwa Fulham. Lakini hali ni tofauti, lazima wachezaji wa kizazi cha sasa waongeze bidii ili kupata mafanikio,"alisema.
Pamoja na hayo, Wome anaamini mafanikio yaliyofikiwa na wachezaji kama George Weah wa Liberia, Samuel Eto'o wa Cameroon, Abedi Pele wa Ghana, Didier Drogba wa Ivory Coast na wengine yanaweza kufikiwa na wachezaji wengine wa Afrika iwapo watatia juhudi.
"Siyo mwisho, safari bado ndefu, lazima watu watie bidii ili kupata mafanikio, nazungumzia kizazi kinachoibuka sasa, kina nafasi ya kurudisha heshima ya wachezaji wa Afrika Ulaya,"alisema.
Kisoka, Wome aliibukia katika klabu ya kwao, Canon Yaounde mwaka 1994 kabla ya kununuliwa na Vicenza ya Italia mwaka 1996, ambayo aliichezea hadi 1997 aliopohamia Lucchese alikocheza hadi 1998 akatua AS Roma, ambako alidumu hadi 1999 alipohamia Bologna.
Wome alihamia England katika klabu ya Fulham mwaka 2002 akitokea Italia ambako alicheza hadi 2003 akahamia Hispania katika klabu ya Espanyol aliyoichezea hadi 2005, akahamia Brescia, baadaye Inter Milan hadi 2006 alipohamia Werder Bremen hadi 2008 alipotimkia FC Koln, ambako alidumu hadi 2011 alipotua Sapins, kabla ya kurejea kumalizia soka yake nyumbani mwaka jana, Coton Sport.
Wome jioni ya leo anatarajiwa kuongoza ukuta wa Cameroon, Simba Wasiofungika katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Tanzania, Taifa Stars kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Huo utakuwa mchezo wake wa 68 kuichezea Cameroon tangu mwaka 1998 na ndani ya mechi hizo, anajivunia kutwaa Medali ya Dhahabu ya Olimpiki mwaka 2000.