Wambura |
ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura kwa mara nyingine amekusudia kwenda Mahakamani iwapo uongozi wa TFF utafanya uchaguzi wa viongozi kwa kutumia kanuni mpya.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo mchana katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Wambura amesema amefikia uamuzi huo baada ya kubaini kufanyika kwa njama ili uchaguzi usifanyike ama uharibike na viongozi waliopo waendelee kuwepo madarakani.
Alisema Katiba iliyotumika kuitisha uchaguzi ni batili kwa kuwa mabadiliko yake hayakufuata utaratibu wa kikatiba kwani hakuna Mkutano Mkuu wowote wa TFF uliokaa kupitisha mabadiliko hayo.
“TFF imempotosha Msajili wa Vyama kupitia ibara ya 76 ya Katiba ya TFF, ya kuwa Mkutano mkuu wa TFF ulikutana Desemba 15, 2012 kufanya mabadiliko hayo huku ikijua sio kweli, ninapenda kuitahadharisha TFF, hili siyo suala la mchezo, ni suala la kisheria.
Hivyo, kwa mujibu wa sheria za nchi, mwenye mamlaka ya kutafsiri sheria (Katiba) ni Mahakama, hivyo ushauri wangu kwa TFF, ili kuondoa uwezekano wa mkono wa sheria kuingia, hawana budi kufuata haya,”alisema.
Mosi, Wambura ametoa pendekezo la kusimamisha matumizi ya Katiba hiyo mara moja, kwani siyo halali, ili kuondoa uwezekano wa kutafutwa haki kwenye Mahakama za dola.
Pili, Wambura ameitaka TFF kuyafuta maamuzi yote na kuivunja Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi inayoongozwa na Iddi Mtinginjola na ili matakwa ya kikatiba ya uchaguzi yatimie, rufaa zote zirudishwe kwenye Kamati ya Rufaa kama Katiba halali inavyotaka, ili kukamilisha mchakato wa uchaguzi.
Tatu, amesema maamuzi yaliyofanywa na Kamati ya uchaguzi chini ya Lyato (Deo-Mwenyekiti wa Kamati) yaheshimiwe na kama kuna wasioridhika wakate rufaa Kamati ya Rufaa ya TFF, pamoja na kuwa maamuzi ya Lyatto hayana maamuzi ya moja kwa moja na yeye, lakini itaweka misingi bora ya kikatiba.
Akifafanua zaidi, Wambura alisema kwa mujibu wa Katiba mpya, ambayo yeye anaiita siyo halali ibara ya 76, Katiba hiyo imeanza kutumika Desemba 15, mwaka jana (2012) na kanuni za uchaguzi zimeanza kutumika Januari 7, mwaka huu (2013), wakati kanuni hizo na Katiba yake ndizo zilizotumika kuitisha uchaguzi mkuu.
“Baada ya kupitisha Katiba mpya na kuanza kutumika, TFF ilipaswa kuunda Kamati mpya ya uchaguzi, kwa mujibu wa Katiba ya TFF ibara ya 49 (4), Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi anapaswa kuwa na taaluma ya Sheria, sifa ambayo Lyatto hana.
“Hivyo ushiriki wake kuwa kinyume na Katiba ya TFF, hali inayoufanya uchaguzi wake kuwa batili na unapaswa kufutwa na kuteua Kamati mpya, ili mchakato uanze upya na hivyo kuchelewesha kupatikana kwa viongozi wapya wa TFF,”alisema
“Kanuni hutengenezwa ili kuwezesha utekelezaji wa Katiba husika, hivyo Katiba hupitishwa na kusajiliwa kwanza na baadaye hutungwa kanuni, cha kushangaza Kanuni za uchaguzi za TFF zilipitishwa na kusainiwa Januari 7, 2013 wakati Katiba ya TFF ilisajiliwa na kugongwa muhuri wa Msajili Januari 10, siku tatu baada ya kanuni kusainiwa.
“Suala linakuja, kanuni hizi zilitungwa kwa mujibu wa Katiba batili kisheria, ninaishauri TFF ili kuondoa uwezekano wa kuiingiza TFF kwenye mgogoro wa kisheria, uamuzi wa busara wa kuachana na Katiba batili ni muhimu kwa maendeleo ya soka Tanzania kwa kusimamisha matumizi ya Katiba mpya batili ya TFF na matokeo ya maamuzi yote yanayotokana na Katiba hiyo,”alisema
Awali, Wambura ambaye alikuwa akigombea nafasi ya Makamu wa Rais katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Februari 24, mwaka huu jina lake lilienguliwa kutokana na sababu kadhaa ikiwemo suala la uadilifu.
Alisema matarajio yake ya kuwania nafasi hiyo, yalianza kuingia dosari kwa mara ya nne, tangu 2008 katika chaguzi mbalimbali ambazo TFF ina maslahi nazo ambako jina lake liliondolewa na Kamati ya uchaguzi kwa sababu mbalimbali.
Uchaguzi wa TFF, umeingia doa, baada ya Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi, kumkata mgombea Urais, Jamal Malinzi kwa madai hana uzoefu. Siku moja baada ya Kamati hiyo mpya kumkata Malinzi, Kamati ya uchaguzi ilisimamisha kampeni zilizokuwa zianze jana hadi hapo itakapotangaza tena baadaye, ingawa Kamati hiyo imesistiza uchaguzi utafanyika kama ulivyopangwa Februari 24, mwaka huu.