Umony |
Na Mahmoud Zubeiry
MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Mganda Brian Umony anaweza kuwemo kwenye kikosi cha timu hiyo kitakachoondoka wiki hii kwenda Sudan Kusini kucheza mechi ya marudiano, Raundi ya Kwanza, Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Nasir Juba.
Mshambuliaji huyo aliyeumia kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Wasudan hao wiki iliyopita, hali yake inaendelea vizuri na jana alifanyiwa vipimo.
“Umony tunaweza kuwa naye kwenye safari ya Sudan Kusini, hali yake inaendelea vizuri,”alisema kocha Msaidizi wa Azam, Muingereza Kali Ongala, alipozungumza na BIN ZUBEIRY.
Azam inahitaji sare au kutofungwa kwa tofauti ya zaidi ya bao moja ili kusonga mbele katika michuano hiyo ya Afrika wanayoshiriki kwa mara ya kwanza.
Hiyo inafuatia Wana Lamba Lamba kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 katika mchezo wa kwanza mjini Dar es Salaam.
Ongala amesema wana matumaini ya kwenda kupata ushindi mnono katika mchezo wa marudiano, kwani timu yao ni bora kuliko Wasudan hao wa Kusini.
“Tunaweza kwenda kushinda ugenini pia, timu yetu ni nzuri kuliko wapinzani wetu. Timu imeendelea na maandalizi kwa ajili ya Ligi Kuu na mechi hiyo, lengo letu ni kufika mbali,”alisema Ongala.