Ulimwengu akiwa mazoezini Stars jana |
Na Mahmoud Zubeiry
MSHAMBULIAJI
wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Thomas Ulimwengu amesema kwamba ana imani
wataifunga Cameroon katika mchezo wa kesho wa kirafiki wa kimataifa, Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY baada ya mazoezi ya jana, Uwanja wa Taifa, Ulimwengu alisema
kwamba kwa kuwa kikosi chao kimekamilika kambini na wachezaji wa ari kubwa,
anaamini watashinda mchezo wa kesho.
Uli,
anayechezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), alisema
kwamba wachezaji wa Tanzania sasa wana uzoefu wa kucheza dhidi ya timu kubwa na
anaamini kesho watashinda.
“Kweli
Cameroon ina wachezaji wengi wanaocheza Ulaya, wazoefu na wazuri hata kiufundi
kuliko sisi, lakini hata sisi kwa maana ya wachezaji wa Tanzania tunabadilika
sana siku hadi siku, hivyo wapenzi watarajie burudani nzuri kesho,”alisema.
Kwa
upande wake, kiungo Simon Msuva alisema kwamba anafurahi sana kuwapo katika
kikosi cha timu ya taifa na kupata mechi za kumkomaza kisoka.
“Mechi
hizi zinamjenga mchezaji, sana tena. Naamini nikipewa nafasi Jumatano nitafanya
vizuri na mashabiki watafurahia,”alisema Msuva, anayechezea Yanga.
Amri
Kiemba alisema kwamba anafurahia umoja uliopo ndani ya timu yao kwa sasa na
hiyo ni chachu ya ushindi kesho.
“Wachezaji
tunakaa vizuri, pamoja na tunapendana, viongozi wanatujali, kwa kweli tupo
katika mazingira mazuri na hii naamini ni chachu ya ushindi kwetu,”alisema
Kiemba, anayechezea Simba SC.
Wachezaji
21 wapo kambini Stars katika hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam ambao ni makipa
Juma Kaseja (Simba), Mwadini Ali (Azam) na Aishi Manula (Azam). Mabeki ni
Erasto Nyoni (Azam), Nassoro Cholo (Simba), Aggrey Morris (Azam), Nadir Haroub
(Yanga), Kelvin Yondani (Yanga), Shomari Kapombe (Simba) na Issa Rashid (Mtibwa
Sugar).
Viungo
ni Amri Kiemba (Simba), Simon Msuva (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Shabani
Nditi (Mtibwa Sugar), Salum Abubakar (Azam), Khamis Mcha (Azam), Athuman Idd
(Yanga) na Mwinyi Kazimoto (Simba). Washambuliaji ni Mrisho Ngasa (Simba), na
Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo (DRC).