Kikosi cha Simba kilichofungwa 1-0 na Libolo Dar es Salaam. Watalipa kisasi na kusonga mbele? |
Na Mahmoud Zubeiry
MKUU wa Msafara wa Simba SC nchini Angola, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba hawaendi nchini humo kukamilisha ratiba, bali wanakwenda kupambana kutaka kurudia historia ya klabu hiyo kugeuza matokeo.
Simba imeondoka Alfajiri ya leo mjini Dar es Salaam kuelekea Angola, kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Recreativo de Libolo, ikiwa nyuma kwa 1-0.
Hans Poppe: Tunakwenda vitani |
“Kweli tulifungwa 1-0 nyumbani, lakini na sisi tuna uwezo wa kwenda kuwafunga kwao, nataka niwahakikishie wapenzi na wanachama wa Simba, hatuendi kukamilisha ratiba, tunakwenda kupambana,”alisema Hans Poppe, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC.
Hans Poppe alisema kwamba katika mchezo wa kwanza, Simba ilitengeneza nafasi ikashindwa kuzitumia, wakati wapinzani wao waliitumia vyema nafasi yao moja muhimu waliyoipata.
“Timu yetu imekuwa kambini kwa muda mrefu, ikijiandaa na tumepata mechi ngumu za Ligi Kuu, ambazo naamini zimetujenga na tuko tayari kupambana kulinda heshima ya klabu,”alisema.
Kwa mujibu wa ratiba ya safari yao, Simba SC watakuwa wametua katika ardhi ya Luanda saa 5:00 asubuhi sawa na saa saa 7:00 za Afrika Mashariki. Baada ya hapo, Wekundu hao wa Msimbazi wataandaliwa utaratibu wa kwenda katika mji wa Calulo, ambako itachezwa mechi hiyo Jumapili.
Wachezaji waliokwenda kuipigania Simba Angola ni pamoja na Nahodha, Juma Kaseja, Abbel Dhaira, Nassor Said ‘Chollo’, Amir Maftah, Juma Nyosso, Shomari Kapombe, Komabil Keita, Salim Kinje, Kiggi Makassy, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto, Haruna Moshi ‘Boban’, Mrisho Ngassa, Ramadhani Chombo ‘Redondo’, Abdallah Seseme, Haruna Chanongo na Abdallah Juma.
Kwa upende wa viongozi, mbali na Hans Poppe, wengine ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Muhsin Balhabou, Kocha Mkuu Mfaransa Patrick Liewig, Kocha Msaidizi Jamhuri kihwelo ‘Julio’ , Kocha wa makipa James Kisaka, Meneja Moses Basena, Daktari Cossmas Kapinga na Mtunza vifaa, Kessy.
Mwaka 1978, Simba iliwahi kufungwa mabapo 4-0 nyumbani na Mufurila Wanderers, lakini ikaenda kushinda 5-0 katika mchezo wa marudiano ugenini Zambia na kusonga mbele katika michuano kama hii na hatua kama hii.