Na Bin Zubeiry |
USHIRIKINA ni moja ya matatizo sugu katika soka ya Tanzania,
ambayo miaka nenda, rudi yameendelea kuwa mstari wa mbele katika kukwamisha
maendeleo ya mchezo huo nchini.
Viongozi wetu, walio wengi wanaamini ushirikina, wachezaji
wetu kadhalika na hili dhahiri limekuwa likiturudisha nyuma sana.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeweka sheria ya
kupambana na imani hizo, lakini kwa kuwa ni sheria iliyolengeshwa katika wigo
mdogo sana kwenye soka yetu, tatizo hili limezidi kukuwa.
TFF hutoa adhabu kwa timu au mtu, iwapo atafanya mambo hayo
hadharani uwanjani na akaonekana, lakini pia bado mambo yenye viashirio vya imani
za kishirikina yamekuwa yakiendelea sana katika viwanja vyetu na shirikisho
hilo linafumbia macho.
Nini maana yake, tatizo hilo linazidi kukua siku hadi siku na
linaongeza vikwazo vya soka yetu kupiga hatua.
Wiki hii imeripotiwa kutokea mtafaruku baina ya wachezaji wa
klabu ya Yanga, wakituhumiana kulogana, mshambuliaji Mrundi, Didier Kavumbangu
akimtuhumu mzalendo Jerry Tegete eti anamloga ndiyo maana hafungi mabao kwa
sasa.
Ikumbukwe baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, Kavumbangu
ndiye alikuwa anaongoza kwa mabao Yanga, lakini katika mzunguko wa pili, mechi
ya kwanza Tegete ameanza kufunga mabao mawili, wakati Kavumbangu hana kitu
ndani ya mechi mbili.
Kweli kuna dalili za wachezaji hawa kushikana uchawi- na si
hao tu, ndani ya Yanga inaonekana wachezaji wengi hawaaminiani.
Suala la ushirikina kwa wachezaji wa Yanga linaonekana kuota
sugu, na wabaya ni wale wanachama walio karibu na wachezaji, kwani ndio
wamekuwa wakipandikiza chuki hizo.
Siku moja niliwahi kumsikia mwanachama mmoja wa kike wa Yanga,
anajisifia kumpeleka kwa mganga Hamisi Kiiza hadi mambo yake yakamnyookea
kwenye timu.
Wapo wanachama pale Yanga hawana shughuli nyingine ya kufanya
zaidi ya kuomba omba fedha kwa wachezaji na viongozi kwa kutumia ujanja wa aina
tofauti, mojawapo ni kuwachonganisha wachezaji wa kuwaambia wanalogana.
Mchezaji kuwa katika kiwango cha juu na wakati fulani kushuka
kidogo, hilo ni jambo la kawaida dunia nzima tangu wakati ule Pele anacheza
soka- kwa sababu soka ni mchezo wa mazoezi na unaohitaji fikra pevu pia ili
kuucheza kwa ufanisi.
Kama mchezaji ametoka kwenye majeruhi, lazima ataanza
taratibu ili kurudi katika hali yake ya kawaida au kama mchezaji ana msongo wa
mawazo, tena ya kibinaadamu tu, amevurugwa kwa namna yoyote, lazima akili yake
itahama uwanjani na hatafanya vizuri.
Basi ikitokea mchezaji hafanyi vizuri kidogo hata kama ana
tatizo la msingi, vidudu mtu wataanza kuingiza fitina ya ushirikina na matokeo
yake wachezaji hawasemeshani.
Hili linasikitisha mno, kwa sababu viongozi wa klabu yetu
wameshindwa kulichukulia hatua na miaka nenda, rudi linazidi kuota mizizi. Pale
Yanga, kuna wachezaji waliachwa eti kwa sababu wanaloga wenzao hawachezi. Waliitwa
wachawi sugu.
Unawezaje kumjua mchawi kama na wewe mwenyewe si mchawi? Said
Maulid ‘SMG’ aliporudi kutoka Angola alipokuwa anacheza soka ya kulipwa,
aliomba kusajiliwa Yanga bure amalizie soka yake pale.
Aliomba hivyo kwa sababu Yanga ni klabu ambayo aliitumikia
kwa mapenzi yake yote kabla hajaenda Angola na alitaka astaafu kwa heshima
hapo. Lakini, akakataliwa na moja ya sababu, amini nakuambia, kuna watu
walimtilia fitina eti atawaumiza wenzake.
Huyu Shadrack Nsajigwa anapigwa vita Yanga aachwe hata leo,
kwa sababu eti anawaumiza wenzake. Hizi ni chuki ambazo zinapandikizwa na kweli
wachezaji wanaishi bila maelewano na upendo katika timu moja.
Mbaya zaidi, malipo duni wanayopata badala ya kufanyia mambo
yao ya maendeleo, nao wanapeleka fedha kwa waganga. Nitawakumbusha kitu kimoja,
kipindi kile damu yangu inachemka kisawasawa, nazama kila chimbo kusaka habari,
niliwahi kukutana na habari moja ya kisa cha mshambuliaji Omar Changa kujitoa
katika klabu ya Yanga.
Niliposikia nilimfuata mchezaji mwenyewe kufanya naye
mahojiano, na kweli akaniambia ameondoka Yanga na harudi tena, kwa sababu
analogwa mchezaji mwenzake Heri Morris. Na kweli Changa hakuwahi kurudi Yanga
na alikuwa mchezaji mzuri sana, ambaye kama angepitia kwenye misingi mizuri
hadi leo angekuwa anacheza soka ya kiwango cha juu tu.
Heri Morris mwenyewe, imani hizo hizo za kishirikina
zimemuondoa uwanjani mapema, wakati alikuwa bonge la mshambuliaji anayejua
kufunga.
Tatizo hili halipo Yanga tu, hadi Simba pia, kuna wachezaji
nawajua waliachwa eti sababu wanawaloga wenzao mfano Emmanuel Gabriel na Ulimboka
Mwakingwe.
Juma Kaseja pale, akija kipa hata akiumia mwenyewe tu na
kushindwa kuendelea kucheza anaambiwa kamshughulikia. Inahitaji moyo sana
kucheza soka Tanzania.
Viongozi wa klabu zetu wanaweza kukomesha hali hii katika
timu zao, kama na wao hawaamini ushirikina, lakini kama unakuwa na kiongozi
naye mshirikina, akisikia malalamiko ya wachezaji kulogana, naye atachochea tu.
Tuna kazi kubwa katika soka yetu, tuanze kumtafuta kiongozi
aliye mweledi, lakini wakati huo huo tumtazame kama si mshirikina, kweli hilo
linawezekana? Ndiyo maana nasema tuna kazi kubwa.
Ipo haja ya viongozi wa soka la Tanzania, kupambana na hizi Imani
za kishirikina ndani ya timu, kwa sababu athari zake tumeziona sasa. Ni kubwa. Mimi
nawajua, wapo wachezaji walicheza zamani kidogo miaka ya 1980 hadi 1990, lakini
hadi leo hawasemeshani kwa madai ya kulogana.
Hili jambo ni hatari kwa kweli na ipo haja kabisa ya kuing’oa
mizizi ya fitina za ushirikina na ushirikina wenyewe katika timu zetu, ili
kuisafisha soka yetu. Hatuwezi kupiga hatua tunayofikiria, ikiwa soka yetu
imesongwa na matatizo ukuki, tutabakia tu kumezea mate mafanikio ya wengine.
Tunahitaji viongozi wasio washirikina, ili kupambana na imani
za kishirikina katika soka yetu. Alamsiki.