Boniface Wambura |
Na Prince Akbar
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) linazitakia kila la kheri timu za Azam, Jamhuri na Simba ambazo zinaiwakilisha Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura Mgoyo amesema leo kwamba, Azam inacheza na Al Nasir Juba ya Sudan Kusini katika mchezo wa Kombe la Shirikisho utakaofanyika Jumamosi (Februari 16 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Nayo Jamhuri ya Zanzibar kesho itacheza na St. Georges ya Ethiopia katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaofanyika Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba. Simba itacheza na Recreativo do Libolo ya Angola keshokutwa (Februari 17 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wakati huo huo: Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limesitisha ukamishna wa Hafidh Ali. Uamuzi huo umefanywa na Kamati ya Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika iliyokutana Januari 17 mwaka huu jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa barua ya Katibu Mkuu wa CAF, Hicham El Amrani kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), ukamishna huo umesitishwa kwa vile hadi sasa Shirikisho hilo halijapata ripoti ya mechi namba 78 kati ya Comoro na Libya ambayo Ali aliteuliwa kuisimamia.
Hivyo, ukamishna wa Ali umesitishwa hadi hapo CAF itakapopokea ripoti kuhusiana na mechi hiyo ambayo ilikuwa ni kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za AFCON zilizofanyika mwaka huu nchini Afrika Kusini.
Katika hatua nyingine, TFF imetoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Wataalamu wa Tiba ya Michezo Tanzania (TASMA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Februari 10 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Wambura amesema ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonyesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TASMA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia tiba ya wanasoka nchini.
Amesema TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya TASMA chini ya uenyekiti wa Dk. Mwanandi Mwankemwa aliyeibuka mshindi katika uchaguzi huo kwa kura 18 dhidi ya 7 za aliyekuwa Mwenyekiti Biyondho Ngome
Amesema uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu kwa kuzingatia katiba ya TASMA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.
Amesema TFF pia inatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya TASMA chini ya Dk. Paul Marealle na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Safu nzima ya uongozi wa TASMA iliyochaguliwa inaundwa na Dk. Mwanandi Mwankemwa (Mwenyekiti), Dk. Nassoro Matuzya (Katibu Mkuu), Sheky Mngazija (Katibu Msaidizi), Dk. Juma Mzimbiri (Mhazini), Joakim Mshanga (mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF) na Dk. Hemed Mziray (mjumbe wa Kamati ya Utendaji).
Ukiondoa nafasi ya Mwenyekiti, wagombea wengine wote hawakuwa na wapinzani. Nafasi ya Makamu Mwenyekiti haikupata mgombea, hivyo itajazwa katika uchaguzi mdogo utakaofanyika baadaye mwaka huu.