Rais wa TFF, Tenga akizungumza na Waandishi wa Habari mchana wa leo Uwanja wa Taifa |
Na Mahmoud Zubeiry
RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Chillah Tenga amesema kwamba wagombea walioenguliwa na Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi wana namna mbili tu za kufanya ili kutafuta haki yao, moja kuomba pingamizi dhidi yao kusikilizwa tena au kwenda Mahakama ya Usuluhishi ya Soka (CAS), iliyo chini ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Akizungumza na Waandishi wa Habari mchana wa leo, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mara baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji ya TFF, Tenga amesema kwamba TFF ilijiwekea utaratibu ambao lazima uheshimiwe.
Alisema mchakato wa uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Februari 24, mwaka huu ulianza vizuri na umeendelea vizuri hadi kufika hapa ulipo, ingawa amekiri kuna matatizo.
Tenga alisema kwamba kwa mujibu wa utaratibu wa TFF, Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ndiyo chombo cha mwisho na mtu anapokwama hapo hana pa kwenda zaidi ya CAS.
Kauli hiyo ya Tenga imefuatia Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi chini ya Mwenyekiti wake Iddi Mtiginjola kumuengua mgombea wa nafasi ya Urais, Jamal Malinzi kwa madai mawili, kukosa uzoefu na kupinga waraka wa mabadiliko ya uchaguzi.
Taarifa ya Mtiginjola Jumatatu, ilisema kwamba mgombea pekee aliyepitishwa katika nafasi ya Urais, inayoachwa wazi na Tenga anayeng’atuka ni Athumani Jumanne Nyamlani.
Malinzi aliwekewa pingamizi awali, lakini akashinda mbele ya Kamati ya Uchaguzi na baadaye akakatiwa Rufaa, ambayo imemuengua.
Nyamlani pia aliwekewa pingamizi, akashinda na akakatiwa Rufaa lakini pia ameshinda, baada ya pingamizi alilowekewa kutupiliwa mbali.
Wengine walioenguliwa ni Michael Wambura aliyekuwa akiwania nafasi ya Makamu wa Rais na Ahmed Yahya aliyekuwa akiwania nafasi ya Uenyekiti wa Bodi ya Ligi.
Hata hivyo, Tenga amesema kwamba tayari Malinzi na Mohamed Yahya wameomba kusikilizwa upya kwa pingamizi dhidi yao.
Kufuatia matatizo haya, Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Jumanne wiki hii iliamua kusimamisha kampeni za uchaguzi wa shirikisho hilo zilizopangwa kuanza Jumatano, kuelekea uchaguzi huo Februari 24, mwaka huu.
Taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Deo Lyatto ilisema kwamba, Kamati yake imechukua hatua hiyo kutokana na Mamlaka iliyonayo Kikatiba.
“1. Kamati ya Uchaguzi, kwa mamlaka iliyonayo, kupitia Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 3(1), 6(1) (g) na (l), 10(5), 11(6) inayosomeka pamoja na Ibara ya 14(1) na (2) na pia Ibara ya 26(5) na (6), imesitisha zoezi la kampeni za uchaguzi wa TFF na TPL Board lililokuwa lianze kesho tarehe 13/02/2013 hadi hapo itakapowatangazia, ili kuhakikisha kuwa mchakato wa uchaguzi unakidhi kikamilifu matakwa ya Kanuni za Uchaguzi na Katiba ya TFF,”imesema taarifa hiyo.
Aidha, Taarifa ya Lyatto imesema; “2. Tarehe za Uchaguzi Mkuu wa TFF na TPL Board zinabaki kama zilivyopangwa. 3. Taarifa hii inazingatia pia Ibara ya 2(4) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF inayoagiza uongozi uliopo madarakani kuendelea na kutekeleza majukumu ya Shirikisho hadi hapo mchakato wa uchaguzi utakapokamilika,”.