Na Prince Akbar
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeupongeza uongozi mpya wa Chama cha Wachezaji Soka Tanzania (SPUTANZA) na wa Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) uliochaguliwa wiki iliyopita.
Uongozi wa FRAT ulichaguliwa Februari 13 mwaka huu mjini Morogoro wakati wa SPUTANZA ulichaguliwa jana (Februari 17 mwaka huu) katika uchaguzi uliofanyika katika hoteli ya Sun Rise Beach Restort, Kigamboni, Dar es Salaam.
Waliochaguliwa kuongoza SPUTANZA na hawakuwa na wapinzani ni Mussa Kissoky (Mwenyekiti) na Said George (Katibu Mkuu) wakati Ali Mayai aliwashinda Isaac Mwakatika na Hakim Byemba katika nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF.
Kusianga Kiata na Charles Mngodo walichaguliwa kuwa Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya SPUTANZA. Katika uchaguzi huo uliohudhuriwa na wapiga kura 17, Mhazini na nafasi moja ya mjumbe wa Kamati ya Utendaji zitajazwa baadaye kutokana na kukosa wagombea.
Kwa upande wa FRAT viongozi waliochaguliwa ni Said Nassoro (Mwenyekiti), Charles Ndagala (Katibu Mkuu) na Kamwanga Tambwe (mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF).
Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza vyama hivyo unaonesha jinsi wapiga kura walivyo na imani kubwa kwao, na TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya FRAT na SPUTANZA.
Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu kwa kuzingatia katiba zao pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yao.
Pia tunatoa pongezi kwa kamati za uchaguzi za FRAT na SPUTANZA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi umeendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Uchaguzi wa SPUTANZA ulifanyika chini ya udhamini wa kampuni ya Kishen Enterprises Limited, iliyo chini ya Mkurugenzi wake, Dilseh Solanki.
Katibu wa SPUTANZA, Said Geirge amesema kwamba baada ya uchaguzi watafanya tuzo za Mwanasoka Bora Tanzania ifikapo Mei, mwaka huu baada ya Ligi Kuu chini ya udhamini wa Kishen.
Aidha, George alisema pia wameanzisha mpango maalum wa kuwasaidia wachezaji wanaokabiliwa na matatizo mbalimbali na wiki hii wataanzia kwa wachezaji wastaafu, Athumani Kilambo na Omar Kapera ambao wanaumwa kwa sasa.
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa SPUTANZA wakiwa katika picha ya pamoja leo mchana baada ya mkutano wao |
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa SPUTANZA, Omar Zimbwe kulia akitazama kamera ya Shaaban Katwila. Nyuma ni Kussi Kihata |
Bosi mpya SPUTANZA, 'Father', Mussa Kisoky |
Kutoka kulia ni Tumaini Mfungo, Boniface Njohole na Hamisi Malifedha |
Kutoka kulia ni Rashid Chama, Isihaka Hassan na Ibrahim Magongo |
Kutoka kulia ni Edwin Hagai, Omar Zimbwe, Shaaban Katwila na Hakim Byemba |