Song |
Na Prince Akbar
MENEJA
wa timu ya soka ya Cameroon, Simba Wasiofungika, Rigobert Song amesema hana
tatizo lolote na Nahodha wa timu hiyo, Samuel Eto’o, bali kuna watu walikuwa
wanawachonganisha ili kuwavuruga.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY jana baada ya kutua nchini tayari kwa mchezo wa kesho dhidi ya
wenyeji, Tanzania, Taifa Stars, beki huyo wa zamani wa Liverpool alisema kwamba
lakini wamekwishagundua hilo na wameketi chini kuzungumza kumaliza tofauti zao.
“Kwa
sasa sisi ni kitu kimoja, tulizungumza tukamaliza tofauti zetu, baada ya kujua
kuna watu walikuwa wanatuchonganisha,”alisema Song.
Akiuzungumzia
mchezo wa kesho, Song alisema kwamba anatarajia kabisa utakuwa mgumu kwa sababu
Tanzania ni timu nzuri japo haina umaarufu kisoka.
“Tanzania
ina wachezaji wazuri, na tumewahi kucheza nao mimi nikiwa uwanjani, nakumbuka
sana nilipambana na wachezaji wazuri, ambao naamini watatupa changamoto nzuri,”alisema.
Cameroon
ilianza kutua jana kwa mafungu, kundi la kwanza lenye watu 13 likiingia nchini saa
4.40 usiku, kundi la pili linaloongozwa na Nahodha, Eto’o linatarajiwa kutua leo
saa 3.45 asubuhi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Eto’o
anayechezea timu ya Anzhi Makhachkala ya Urusi atatua kwa ndege ya Kenya
Airways akiwa na Herve Tchami wa Budapest Honved ya Hungary, beki Nicolas
Nkoulou wa Marseille ya Ufaransa, mshambualiji Jean Paul Yontcha wa SC
Olhanense ya Ureno na daktari wa timu Dk. Boubakary Sidik.
Saa
moja baadaye baada ya Eto’o kutua na wenzake, Kocha wa timu hiyo Jean Paul
Akono na msaidizi wake Martin Ndtoungou watawasili saa 4.40 asubuhi kwa ndege
ya Kenya Airways wakitokea Afrika Kusini.
Leo
pia kuna kundi lingine litakaloingia saa 4.40 usiku kwa ndege ya KLM ambalo
lina beki Jean Kana Biyick wa Rennes ya Ufaransa, mshambuliaji Fabrice Olinga
wa Malaga FC ya Hispania, beki Allan Nyom wa Udinese ya Italia ambaye yuko kwa
mkopo Granada ya Hispania na beki wa kushoto Henri Bedimo wa Montpellier ya
Ufaransa.