Beki wa Simba, Amir Maftah akiokota mpira nyavuni baada ya Salvatory Ntebe kuifungia Mtibwa bao pekee la ushindi. Kulia ni kipa wake Juma Kaseja. |
SIMBA SC imezidi kupoteza matumaini ya kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya jioni ya leo kulala bao 1-0 mbele ya Mtibwa Sugar ya Morogoro kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mbaya wa Simba SC leo alikuwa ni beki Salvatory Ntebe, aliyefunga bao hilo pekee la ushindi dakika ya 18 kwa guu lake la kulia, akiunganisha krosi maridadi ya winga wa zamani wa Yanga, Vencent Barnabas.
Simba SC walionekana kuzidiwa na Mtibwa, haswa katika safu ya kiungo, ambako timu hiyo ya Manungu, ilikuwa ina mafundi kama Rashid Gumbo, Shaaban Kisiga na Shaaban Nditi.
Aidha, mashambulizi ya pembeni, upande wa kushoto, ambako walikuwa wanacheza Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ beki na Barnabas mshambuliaji, yaliitia misukosuko mno ngome ya Simba.
Salvatory Nteve: Mfungaji wa bao |
Simba SC hawakuwa na shambulizi a kushitua dakika 45 za kipindi cha kwanza, zaidi kipa Juma Kaseja alifanya kazi ya ziada kuokoa kuinusuru timu yake.
Kocha Mfaransa wa Simba SC, Patrick Liewig alimtoa uwanjani Redondo baada ya dakika 40 tu na kumuingiza Kiggi Makassy, ambaye kidogo ‘aliifufua’ timu kwa kasi yake.
Kipindi cha pili, Simba ilifanya mabadiliko katika safu ya ushambuliaji ikiwatoa kwa wakati tofauti Haruna Moshi ‘Boban’ na Haruna Chanongo na kuwaingiza Mrisho Ngassa na Amri Kiemba.
Mabadiliko hayo yalileta uhai kidogo katika safu ya ushambuliaji ya Wekundu wa Msimbazi, lakini unaweza kusema hata bahati haikuwa yao leo, kwani walikosa mabao mawili ya wazi, moja Ngassa na lingine Kiggi.
Beki wa Simba Juma Nyosso alitolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 85, baada ya kumpiga Barnabas akiwa hana mpira na tayari refa amepuliza filimbi.
Kutoka kwa Nyosso kuliitibulia Simba kasi ya kusaka bao la kusawazisha, kwani ilibidi waimarishe ulinzi kuepuka kufungwa mabao zaidi.
Ushindi huo, unaifanya Mtibwa itimize pointi 27, baada ya kucheza mechi 18 na kupanda hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu, wakati Simba inabaki nafasi ya tatu kwa pointi zake 31, baada ya kucheza mechi 18 pia.
Yanga inaendelea kuongoza ligi hiyo kwa pointi zake 39, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 36.
Katika mchezo wa leo, kikosi cha Simba SC kilikuwa; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Juma Nyosso, Komabil Keita, Shomary Kapombe, Haruna Chanongo/Mrisho Ngassa dk58, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Haruna Moshi/Amri Kiemba dk 50 na Ramadhan Chombo ‘Redondo’/Kiggi Makassy dk 40.
Mtibwa Sugar; Hussein Sharrif ‘Cassillas’, Said Mkopi, Issa Rashid, Salvatory Ntebe, Salum Sued, Shaaban Nditi, Jamal Mnyate/Ally Mohamed ‘Gaucho’ dk49, Rashid Gumbo, Hussein Javu/Juma Liuzio dk84, Shaaban Kisiga na Vincent Barnabas.