Milovan kulia akisalimiana na Liewig |
Na Princess Asia
SIMBA SC imesema kwamba haina mpango wa kumrejesha Kocha Mserbia, Profesa Milovan Crikovick na haihusiki na ujio wake hapa nchini.
Msemaji wa klabu ya Simba, Ezekiel Kamwaga ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, klabu hiyo haihusiki na ujio na Milovan hapa.
Alipoulizwa kuhusu kama ana madai dhidi ya klabu, Kamwaga alikiri lakini akasema hajawataarifu kama anakuja kwa ajili ya madai yake.
"Kulipwa lazima alipwe, lakini hawezi kuja tu ghafla na kutaka alipwe, lazima taratibu zifuatwe,"alisema.
BIN ZUBEIRY inatambua Milovan anawadai Simba SC dola za Kimarekani 24, ambazo ni mishahara ya miezi mitatu kabla ya kutupiwa virago Novemba mwaka jana.
Milovan, aliyetimuliwa Simba SC baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, jana aliibuka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati wa mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya Tanzania na Cameroon na kuteka hadhira.
Profesa Milovan aliwapungia mkono mashabiki wa Simba ambao walimjibu kwa shangwe zito na baadaye Milovan, aliwasalimia baadhi ya wadau na kwenda kuketi kushuhudia mchezo huo. Wakati wa mapumziko, alikwenda kusalimiana na kocha aliyerithi nafasi yake, Mfaransa Patrick Liewig.
Tayari zilianza kuibuka hisia kwamba, Mserbia huyo anarejeshwa kazini kwa kuwa kocha wa sasa, Mfaransa Patrick Liewig ameingia kwenye mgogoro na wachezaji 'mafaza' wa Simba SC.