Kikosi cha Simba SC |
Na Dina Ismail
UONGOZI wa klabu ya Simba unatarajiwa kwenda nchini Uingereza kwa ajili ya kukutana na uongozi wa timu ya Sunderland inayoshiriki Ligi Kuu ya huko, ili kuzungumza ushirikiano.
Aidha, Simba imemshukuru Rais wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ambaye alimkutanisha Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage na Mwenyekiti wa Sunderland, Ellis Short ambaye alikuja nchini.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo, Ofisa Habari wa Simba Ezekiel Kamwaga alisema kwamba hatua ya uongozi wa Simba kwenda huko inafuatia hatua nzuri ya mazungumzo ya ushirikiano baina ya pande hizo mbili.
“Kwa kweli tunamshukuru sana Rais Kikwete kwa kumkutanisha Mwenyekiti wetu Rage na Short na ndipo mambo haya mazuri yakajitokeza,”alisema
Alisema ni matarajio yao klabu ya Simba itapiga hatua kubwa kupitia ushirikiano na timu hiyo kongwe nchini Uingereza kwani tayari wameshaanza kukubaliana baadhi ya mambo ikiwemo uendelezaji wa soka la vijana.
Kamwaga aliongeza kuwa uongozi wa Simba utakapokuwa nchini Uingereza pamoja na kushuhudia baadhi ya mechi za timu hiyo, pia utapata fursa ya kubadilishana uzoefu wa kiuongozi na wenyeji wao.
Wakati huo huo; kikosi cha Simba kinatarajiwa kuwasili leo kutoka Arusha kilipokuwa kimepiga kambi, kiingilio cha chini cha mchezo wake wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Recretivo de Libolo ya Angola kimepangwa kuwa Sh. 5, 000.
Timu hizo zinatarajiwa kukwaana Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, mjini Dar es Salaam na kiingilio hicho kitahusisha mashabiki watakaokaa viti vya rangi ya kijani na bluu.
Alivitaja viingilio vingine ni Sh 10, 000 kwa viti vya rangi ya chungwa, Sh 15,000 kwa watakaokaa VIP C, Sh 20,000 kwa VIP B na Sh 30, kwa VIP A.
Kamwaga alisema kwamba kikosi cha Simba kitakapowasili kitaweka kambi katika hoteli ya Spice, iliyopo katika ya jiji kuendelea na maandalizi yake.
Alisema wachezaji wote ukiacha majeruhi Felix Sunzu na Paul Ngalema, wapo katika hali nzuri na na wanaendelea na mazoezi.