Kiungo wa Simba, Amri Kiemba akiwapiga chenga beki Jimmy Shoji na kipa Shaaban Dihile, kabla ya kuifungia bao la kuongoza Simba SC. |
Na Mahmoud Zubeiry
MABINGWA
watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simba SC leo wamelazimishwa sare
ya kufungana bao 1-1 na JKT Ruvu ya Pwani katika mchezo wa Ligi Kuu uliofanyika
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Matokeo
haya yanaiongezea pointi moja tu Simba SC na sasa imetimiza 27, baada ya
kucheza mechi 15, ikiendelea kushika nafasi ya tatu, nyuma ya Azam yenye 30 na
Yanga 33.
Hadi
mapumziko, Simba walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na kiungo Amri
Ramadhan Kiemba, aliyewapiga chenga beki Jimmy Shoji na kipa Shaaban Dihile
dakika ya 17, kabla ya kutumbukiza mpira nyavuni.
Kwa
ujumla Simba walicheza vema kipindi cha kwanza, wakitawala safu ya kiungo na
gonga zao safi za uhakika na kama wangekuwa makini wangeweza kutoka uwanjani
baada ya nusu hiyo ya kwanza wakiwa na hazina kubwa ya mabao.
Kipindi
cha pili mchezo ulibadilika na zaidi Simba ilionekana kuathiriwa na mabadiliko
ya wachezaji iliyomfanya, haswa kumtoa Mrisho Ngassa aliyekuwa akiisumbua ngome
ya JKT.
Maafande
hao wa Ruvu walizidisha kasi ya mashambulizi langoni mwa Simba, wakiamini
Wekundu wa Msimbazi hawana mtu hatari mbele.
Hilo
liliisaidia timu hiyo kupata bao la kusawazisha dakika ya 63, lililofungwa na
Nashon Naftali akiunganisha krosi ya Mussa Hassan Mgosi.
Baada
ya kufungwa bao hilo, Simba walicharuka kusaka bao la ushindi, lakini jitihada
zao ziliishia kwenye ngome ya JKT iliyokuwa imara kipindi cha pili na kutorudia
makosa ya kipindi cha kwanza.
Refa
Alex Mahagi wa Mwanza aliwapa Simba penalti dakika ya 87, baada ya beki Damas
Makwaya kugongana na Haruna Moshi ‘Boban’ kwenye eneo la hatari.
Nahodha
Msaidizi wa Simba SC, Shomary Kapombe alikwenda kupiga penalti yake vizuri,
lakini kipa Shaaban Dihile aliipangua ikagonga mwamba na kurudi uwanjani,
akaichupia kuidaka.
Simba
SC hawakukata tamaa hata baada ya kukosa penalti dakika za lala salama,
waliendelea kufanya mashambulizi ya haraka haraka kusaka bao, lakini bahati haikuwa yao.
Katika
mchezo huo, kikosi cha Simba SC kilikuwa; Juma Kaseja, Haruna Shamte, Paul
Ngalema, Shomary Kapombe, Komabil Keita, Abdallah Seseme/Haruna Moshi, Haroun
Chanongo, Mwinyi Kazimoto, Mrisho Ngassa/Abdallah Juma, Amri Kiemba, Ramadhan
Chombo/Kiggi Makassy.
JKT
Ruvu; Shaaban Dihile, Credo Mwaipopo, Kessy Mapande, Kisimba Luambano, Damas
Makwaya, Jimmy Shoji, Hussein Bunu, Nashon Naftali, Mussa Mgosi, Zahor Pazi na
Emmanuel Pius.