Shujaa wa Stars leo, Samatta |
Na Mahmoud Zubeiry
MBWANA Ally Samatta, jioni hii ameibuka shujaa wa taifa, baada ya kuifungia Tanzania, Taifa Stars bao pekee la ushindi katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Cameroon Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mpira uko nyavuni, Samatta anachomoka kushangilia |
Sama Goal alitumia akili ya hali ya juu kufunga bao hilo, baada ya kuwekewa ulinzi mkali kwa muda wote wa mchezo, kwani alifanya kama hawanii mpira na ghafla akauchomokea, wakati mabeki wa Simba Wasiofungika, wakidhani kipa wao atauwahi.
Aidha, kwa bao hilo tamu, ni sawa na Samatta au Poppa kuwaomba radhi mashabiki kwa kitendo chake cha kususia kambi ya timu iliyokuwa ikijiandaa kucheza na Zambia.
Huu ni ushindi wa tatu mfululizo wa nyumbani kwa Taifa Stars, baada ya awali kuzifunga Kenya Novemba na Zambia Desemba, zote 1-0.
Stars ingeweza kuondoka na ushindi mnene leo, iwapo beki Erasto Nyoni angefunga penalti dakika ya 25, lakini kipa Komguep aliipangua.
Penalti hiyo ilitolewa na refa Munyemana Hudu wa Rwanda baada ya beki Ngoula kumuangusha Samatta kwenye eneo la hatari.
Katika mchezo wa leo, kikosi cha Tanzania kilikuwa; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Shomary Kapombe, Kevin Yondan, Aggrey Morris, Salum Abubakar, Mrisho Ngassa, Frank Domayo, Mbwana Samatta, Mwinyi Kazimoto/Thomas Ulimwengu na Amri Kiemba.
Cameroon; Effala Komguep, Assou Ekotto, Aminou Bouba, Ngoula/Maukon Jean, Nyom Allan, Pierre Wome, Kingue Mpondo, Bedimo Henri/Ashu Glovis, Tchami Herve/Eloundu, Olinga Fabrice/Edoa Charle na Abubakar Vincent/Bakinde Gerard.