|
REFA wa Tunisia, Slim Jdidi amefungiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baada ya kuboronga katika Nusu Fainali ya jana Kombe la Mataifa ya Afrika kati ya Burkina Faso na Ghana.
"CAF haikufurahishwa na kiwango cha uchezeshaji wa mechi," alisema Katibu Mkuu, Hicham El Amrani leo alipozungumza na Waandishi wa Habari."Tunafahamu wanaweza kufanya makosa, lakini tunatarajia kiwango kizuri na urefa,"aliongeza.
Miongoni mwa blanda alizofanya katika mechi hiyo ya jana mjini Nelspruit, ilikuwa ni kadi nyekundu aliyompa mshambuliaji wa Burkina Faso, Jonathan Pitroipa ambaye atakosa fainali Jumapili dhidi ya Nigeria.
Pitroipa alipewa kadi ya pili ya njano katika dakika za nyongeza baada ya kuanguka kwenye eneo la penalti.
Kamati ya Mashindano itaamua kesho kama mchezaji huyo atacheza fainali au la na tayari Burkina Faso imemkatia rufaa refa huyo.
Jdidi pia aliwapa penalti laini mno Ghana katika mechi hiyo, ambayo Burkina Faso hatimaye ilishinda kwa penalti 3-2 baada ya sare ya 1-1.