Kim katikati akizungumza na Waandishi mchana wa leo, kulia Nahodha Juma Kaseja na kushoto, Katibu wa TFF, Angetile Osiah |
Na Mahmoud Zubeiry
KOCHA
Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mdenmark Poulsen
amesema kwamba anataka mechi ngumu zaidi ili kujenga timu imara ya kuwania
tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil.
Akizungumza
katika Mkutano na Waandishi wa Habari mchana huu kwenye ukumbi wa mikutano wa Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF), Pouslen alisema kwamba yuko tayari kwa mchezo wowote
dhidi ya timu ngumu kwa ajili ya kuimarisha kikosi chake.
Kaseja akizungumza na Waandishi leo TFF |
Poulsen
alisema kwamba ameiandaa vyema timu yake kwa ajili ya mchezo wa kesho na vijana
wake wameonyesha kabisa wako tayari kwa mechi hiyo, inayotarajiwa kuwa kali na ya
kusisimua.
“Tulikuwa
tuna mazoezi mazuri jana, wachezaji wote wameripoti na wako vizuri,
wanafahamiana na wamecheza baina yao, Mtibwa Sugar, Yanga na Azam, wanapeana
changamoto. Wanapendana. Napenda sana kaulimbiu ya Umoja ni nguvu, wachezaji ni
wamoja, sisi wote ni wamoja”alisema.
Poulsen
alisema kwamba wachezaji wake wanajua wanatakiwa kucheza vizuri kesho, ili kuwapa
changamoto Cameroon katika mchezo huo, ambao mashabiki wanausubiri kwa hamu.
Kim
alisema wananawaheshimu Cameroon ni timu nzuri na kubwa, yenye wachezaji
wazuri, lakini hilo haliwazuii kusema watashinda mechi ya kesho.
“Tunaamini
staili yetu ya uchezaji itatupeleka katika zama nyingine. Mtindo wetu ni kupiga
pasi kwa wingi na kutengeneza nafasi na kufunga, tukicheza kwa haraka. Na hata
tukipoteza mpira, tunajituma wote kuutafuta. Nina uhakika wachezaji wako tayari
kwa mechi,”alisema.
Kwa
upande wake, Nahodha wa timu hiyo Juma Kaseja amesema kwamba wako tayari kwa
mchezo huo na wanaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi uwanjani kesho kuiunga
mkono timu yao.
“Sisi
wote ni Watanzania, na wote tunahitaji furaha, wenyewe watakuwa 11 na sisi
tutakuiwa 11 na tunatarajia utakuwa mchezo mzuri, mgumu na tutaonyesha kile
tulichokionyesha kwenye mchezo uliopita na Zambia,”alisema Kaseja.
Wachezaji
21 wapo kambini Stars katika hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam ambao ni makipa
Juma Kaseja (Simba), Mwadini Ali (Azam) na Aishi Manula (Azam). Mabeki ni
Erasto Nyoni (Azam), Nassoro Cholo (Simba), Aggrey Morris (Azam), Nadir Haroub
(Yanga), Kelvin Yondani (Yanga), Shomari Kapombe (Simba) na Issa Rashid (Mtibwa
Sugar).
Viungo
ni Amri Kiemba (Simba), Simon Msuva (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Shabani
Nditi (Mtibwa Sugar), Salum Abubakar (Azam), Khamis Mcha (Azam), Athuman Idd
(Yanga) na Mwinyi Kazimoto (Simba). Washambuliaji ni Mrisho Ngasa (Simba), na
Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Cameroon
ilianza kutua jana kwa mafungu, kundi la kwanza lenye watu 13 likiingia nchini
saa 4.40 usiku, kundi la pili linaloongozwa na Nahodha, Eto’o linatarajiwa kutua
leo saa 3.45 asubuhi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
(JNIA).
Eto’o
anayechezea timu ya Anzhi Makhachkala ya Urusi atatua kwa ndege ya Kenya
Airways akiwa na Herve Tchami wa Budapest Honved ya Hungary, beki Nicolas
Nkoulou wa Marseille ya Ufaransa, mshambualiji Jean Paul Yontcha wa SC
Olhanense ya Ureno na daktari wa timu Dk. Boubakary Sidik.
Saa
moja baadaye baada ya Eto’o kutua na wenzake, Kocha wa timu hiyo Jean Paul
Akono na msaidizi wake Martin Ndtoungou watawasili saa 4.40 asubuhi kwa ndege
ya Kenya Airways wakitokea Afrika Kusini.
Leo
pia kuna kundi lingine litakaloingia saa 4.40 usiku kwa ndege ya KLM ambalo
lina beki Jean Kana Biyick wa Rennes ya Ufaransa, mshambuliaji Fabrice Olinga
wa Malaga FC ya Hispania, beki Allan Nyom wa Udinese ya Italia ambaye yuko kwa
mkopo Granada ya Hispania na beki wa kushoto Henri Bedimo wa Montpellier ya
Ufaransa.
Taifa
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itacheza na Morocco, Machi 24
mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ikiwa inashika nafasi ya pili katika
kundi lake kuwania tiketi ya Brazil mwakani, nyuma ya Ivory Coast inayoongoza.
Timu nyingine katika kundi hilo ni Gambia.