// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); POLE YAKE BABU MFARANSA SIMBA SC, KAZI ANAYO! - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE POLE YAKE BABU MFARANSA SIMBA SC, KAZI ANAYO! - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Wednesday, February 06, 2013

    POLE YAKE BABU MFARANSA SIMBA SC, KAZI ANAYO!

    Na Bin Zubeiry

    IMERIPOTIWA kocha Mfaransa wa Simba SC, Patrick Liewig amesema hawataki baadhi ya wachezaji nyota wa timu hiyo, kwa sababu hawana nidhamu.
    Hao ni pamoja na Mrisho Ngassa, Mwinyi Kazimoto na Haruna Moshi.
    Sababu haswa za msingi za Mfaransa huyo aliyeanza kazi mapema mwezi uliopita kuwakinai wachezaji hao hajaziweka wazi, bali amejumuisha tu hawana nidhamu.
    Liewig anaona bora kuwainua wachezaji vijana wa timu hiyo, waliopandishwa kutoka kikosi cha pili watamfanyia kazi nzuri, lakini si magwiji hao.
    Baada tu ya mchezo wa kwanza wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara niliandika kwenye safu hii juu ya hatari inayoweza kumkuta Mfaransa huyo muda si mrefu.
    Nilielezea mfumo anaotaka kuutumia wa kasi na wachezaji wote kujituma uwanjani, unahitaji mazoezi mengi ili wachezaji kuumudu. Nikasema wachezaji wetu wengi hawapendi mazoezi magumu na akitokea mwalimu wa hivyo, watamfanyia zengwe ang'oke.
    Nikasema kocha huyu anahitaji sapoti ya uongozi ili kujenga nidhamu ya uwajibikaji ndani ya timu, vinginevyo Simba hawatafanikiwa. Watabakia kugombea ubingwa wa Bara na Kombe la Mapinduzi, lakini kwenye michuano ya Afrika wataendelea kuvurunda.
    Inafahamika wazi, wanadamu wengi wanapenda pepo, lakini huwezi kwenda peponi kabla ya kufa. Na wachezaji wetu lazima wajiulize, watawezaje kucheza vizuri ikiwa hawako fiti kwa asilimia 100?
    Wachezaji wengi waliofanya vizuri miaka ya nyuma, wamekuwa wakiwaponda wachezaji wa siku hizi, kwa mambo mengi tu, kiufundi hata uimara wa kimchezo.
    Tanzania hatuna mchezaji ambaye angalau anacheza kwa asilimia 70, hata hao akina Mbwana Samatta na Mrisho Ngassa, bado sana. Lakini kwa kuwa kwa kiwango cha hapa hao ndio wanafanya vizuri hivi sasa, ndiyo maana hao ndio mastaa. 
    Ukweli ni kwamba, mambo ya ajabu yaliyofanywa na wachezaji wetu wa miaka ya 1990 tu kama Edibily Lunyamila, sahau kuhusu Zamoyoni Miogella, huwezi kuyaona leo.
    Hii inatokana na kwamba, wachezaji wetu hawajitambui. Na kwa sababu wamekulia katika mazingira hayo, ni vigumu kuwabadilisha mara moja.
    Upo umuhimu wa kujenga misingi mipya imara ya kuibeba soka ya soka Tanzania- kwa kuwekeza kwenye soka ya vijana, nini maana yake, naungana na mipango ya Liewig.
    Hata hivyo, hiki anachotaka kukifanya kwa sasa sina hakika kama mashabiki wa Simba siyo tu watamuelewa, bali kama watakubaliana naye.
    Yanga waliweza mwaka 1995 kuvunja timu nzima na kuunda mpya kabisa kwa kutumia wachezaji wa kikosi cha pili, ambayo mwaka mmoja baadaye ilifika Robo Fainali ya Kombe la Washindi la Afrika.      
    Nadhani wengi wanaikumbuka ile Yanga Black Star, chini ya marehemu Tambwe Leya mwalimu, iliyoibua nyota kama Anwar Awadh, Maalim Saleh, Nonda Shabani, Mzee Abdallah, Omar Kapilima na wengineo.
    Hata Simba, inawezekana pia, kwa sababu tumeona uwezo wa wachezaji vijana katika mashindano mbalimbali, kuanzia Kombe la Banc ABC mwaka jana, Kombe la Mapinduzi na hata Ligi Kuu. 
    Narudia kusema, Simba ina hazina nzuri mno ya wachezaji vijana, ambao wanaweza kumvutia kocha yoyote duniani. Siwezi kuwalaumu akina Ngassa, Boban na Kazimoto kwa sababu sijui malezi yao kisoka na sishangai wakituhumiwa hawana nidhamu.
    Na siwezi kubisha kwamba hawana nidhamu, kwa sababu hata sisi Waandishi wa Habari mara nyingi tumekuwa tukionja joto ya jiwe kutoka kwao.
    Simba iliporejea kutoka Oman, pale Uwanja wa Ndege wachezaji wote hao 'mafaza' waliwakwepa Waandishi ili wasipigwe picha wakatoka kwa kutoroka toroka.
    Ile ilitokana na uelewa wao mdogo, malezi mabaya wanayoendelea kuyapata hadi katika klabu yao hivi sasa.
    Simba inajiendesha pamoja na kwa michango ya wanachama wake, lakini pia kutokana na fedha za mdhamini wao, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), ambaye manufaa anayoyapata ni kutangazwa na wachezaji hao.
    Sasa, kitendo cha kutoka Uwanja wa Ndege wanakimbia kamera saa ngapi matangazo ya Kilimanjaro Beer yatapamba kurasa za magazeti na vioo vya Televisheni kupitia wao?
    Lakini pia, mashabiki wa Simba nchi nzima walitamani kuwaona vyema wachezaji wao wakirejea kutoka ziara hiyo ya Oman, waliwaonaje wakati walitoroka kamera?
    Simba ilitua Oman wachezaji hawana sare, yaani haikuwa kama timu- unaweza kuona matatizo haya yanaanzia kwenye uongozi, kushindwa kuweka taratibu au kuzisimamia kama wameweka. Lakini mwisho wa siku, haya ni mambo ya aibu kwa klabu na kwa taifa, ambayo lazima tuepukane nayo.
    Leo Liewig anataka kupambana na nidhamu ya wachezaji wa Simba, uwezekano wa kushinda ni mdogo sana ikiwa tayari kuna kiongozi amesema, iwapo wachezaji hao watasimamishwa, naye atajiuzulu.
    Lakini tunaipeleka wapi soka yetu. Hili ni la kujiuliza. Kwa sababu za kinidhamu, Azam iliwasimamisha wachezaji wake wanne, lakini hadi leo baadhi yao wameendelea kuitwa timu ya taifa.
    Leo Simba iwafukuze Kazimoto, Ngassa na Boban, wazi Yanga na Azam watachaniana mashati kuwania saini zao.
    Simba itapoteza na ingawa wachezaji hao kama kweli ni tatizo hawatabadilika, lakini kulingana na upinzani uliopo baina ya Simba na Yanga, itakuwa taabu kwa Wekundu wa Msimbazi.
    Na Simba itapata wapi ujasiri wa kuwafukuza wachezaji walio katika timu ya taifa, huku ikijua fika kwa sera ya kocha wa sasa wa timu hiyo, Mdenmark Kim Pouslen hawatapoteza siti zao kwenye timu hiyo?
    Tuna kazi kubwa! 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: POLE YAKE BABU MFARANSA SIMBA SC, KAZI ANAYO! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top