Niyonzima akiwapungia mikono mashabiki baada ya mechi |
Na Mahmoud Zubeiry
KWA mara ya pili mfululizo, kiungo Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima leo tena amekuwa shujaa wa timu yake, Yanga SC baada ya kuifungia bao pekee la ushindi katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Niyonzima alijikuta akituzwa fedha na mashabiki wa timu yake baada ya mechi hiyo, iliyokuwa ngumu kwa Wana Jangwani, kutokana na kuibeba timu hiyo mara mbili mfululizo kwa kufunga mabao ya juhudi binafsi, ikiwemo mechi iliyopita dhidi ya Azam FC.
Didier Kavumbangu akipiga shuti langoni mwa Kagera mbele ya mabeki wa Kagera |
Kagera inabaki na pointi zake 28 katika nafasi ya tano, baada ya kucheza mechi 19, chini ya Coastal Union ya Tanga inayoshika nafasi ya nne kwa pointi zake 30.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Simon Mberwa kutoka Pwani, aliyesaidiwa na Milambo Tshikungu wa Mbeya na Said Tibabimale kutoka Mwanza, hadi mapumziko, hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake.
Hata hivyo, mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Didier Kavumbangu aliikosesha timu yake bao, baada ya kupiga juu ya lango mkwaju wake wa penalti dakika ya 44.
Refa Mberwa, alitoa penalti hiyo baada ya Kavumbangu mwenyewe kudakwa miguu kwenye eneo la hatari na kipa wa Kagera, Mganda Hannington Kalyesebula.
Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko, Yanga inayofundishwa na Mholanzi, Ernie Brandts ikiwatoa Kavumbangu na Bahanuzi na kuwaingiza Jerry Tegete na Mganda Hamisi Kiiza, wakati Kagera inayofundishwa na mzalendo, Abdallah Kibadeni, iliwatoa Mnigeria Darlington Enyinna na Julius Mrope na kuwaingiza Paul Ngway na Themi Felix.
Mabadiliko hayo yaliongeza uhai kwa kila upande na kuongeza kasi na ladha ya mchezo, lakini bahati hii leo ilikuwa kwa wana Jangwani, kutokana na kupata bao pekee la ushindi lililofungwa na kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Niyonzima.
Niyonzima alifunga bao hilo dakika ya 65, baada ya kumhadaa kiungo wa Kagera, George Kavilla na kufumua shuti kali akiwa umbali wa mita 25, lililomshinda kipa wa Kagera, Kalyesebula.
Halikuwa na tofauti sana na bao pekee la ushindi alilofunga kwenye mchezo uliopita wa timu yake dhidi ya Azam FC, Uwanja huo huo wa Taifa, Jumamosi iliyopita.
Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Shijja Mkinna alikosa bao la wazi dakika ya 89, baada ya kupewa pasi nzuri na Paul Ngway, lakini akapiga juu ya lango.
Hiyo ilikuwa nafasi pekee ya kujutia kwa Kagera ambao leo iliitoa jasho Yanga. Jerry Tegete naye alikosa bao la wazi dakika ya 87, akishindwa kuunganisha krosi ya Simon Msuva.
Kwa ushindi huo, Yanga imelipa kisasi cha kufungwa 1-0 na Kagera katika mchezo wa kwanza wa ligi hiyo, mwishoni mwa mwaka jana mjini Bukoba.
Katika mchezo huo, kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva, Frank Domayo, Didier Kavumbangu/Hamisi Kiiza dk67, Said Bahanuzi/Jerry Tegete dk 67 na Haruna Niyonzima.
Kagera Sugar; Hannington Kalyesebula, Benjamin Asukile, Martin Muganyizi, Malegesi Mwangwa, Amandus Nesta, Gaorge Kavilla, Julius Mrope/Paul Ngway dk 62, Juma Nade, Darlington Enyinna/Themi Felix dk 69, Shijja Mkinna na Daudi Jumanne.