Mama Rahma akiwa na Simba Oman |
Na Princess Asia
WANACHAMA wa klabu ya Simba SC, wametakiwa kufika Uwanja wa Ndege
wa Mwalimu Julius Nyerere Februari 10, mwaka huu kumpokea mfadhili wao wa ziara ya Oman, Mama Rahma
Al Kharoos, Malkia wa Nyuki, anayetarajiwa kutua nchini siku hiyo.
Ofisa
Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba,
wanachama na wapenzi wa klabu hiyo wanatakiwa kufika Uwanja wa Ndege wa
kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam siku hiyo kumpokea mfadhili huyo.
“Mama
huyu ametusaidia sana kwa kweli, katika kambi yetu ya Oman alitumia zaidi ya
Sh. Milioni 80 ambazo ziliisaidia sana timu kwa maandalizi, kwa hiyo tunaomba
twende tukampokee, ili kulipa fadhila kwake,”alisema Kamwaga.
Kamwaga
alisema kwamba Mama Rahma atakuwa Mkuu wa Msafara wa Simba itakapokwenda nchini
Angola kucheza na Libolo ya huko katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kabla
ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu wiki iliyopita, Simba iliweka kambi
ya wiki mbili kujiandaa na hatua hiyo kwa ufadhili kamili wa Malkia wa Nyuki.
Hayo yalikuwa majibu kwa wapinzani wao wa jadi, Yanga SC walioweka kambi ya wiki
mbili pia nchini Uturuki.
Matunda
ya ziara ya Oman ni Simba kuanza Ligi Kuu ya kishindo ikiitandika 3-1 African
Lyon na keshokutwa itaingia kwenye mchezo wa pili kusaka pointi dhidi ya JKT
Ruvu ya Pwani.