Mfadhili wa Simba SC, Mama Rahma Al Kharoos, akizungumza na Waandishi wa Habari mchana wa leo katika hoteli ya Movenpick, Dar es Salaam mchana wa leo. |
Na Mahmoud Zubeiry
MFADHILI wa Simba SC, Bi Rahma Al Kharoos, amejitolea kulipa malimbikizo ya mishahara ya miezi mitatu ya aliyekuwa kocha wa klabu hiyo, Mserbia, Profesa Milovan Cirkovick, dola za Kimarekani 24,000 (kiaisi cha Sh Milioni 40,000).
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo mchana katika hoteli ya Movenpick, Dar es Salaam, Rahma maarufu kama Malkia wa Nyuko, amesema kwamba amejitolea kumlipa kocha huyo kwa mapenzi yake kwenye klabu hiyo na kwa kuwa pia aliitumikia klabu, hivyo anadai haki yake.
“Sasa hivi kuna matatizo mengi, kwa hiyo timu haifanyi vizuri, wanachama hawajui waangalie nini, waaangalie matatizo ya kocha aliyetoka anadai fedha zake, au waaangalie timu kwa nini haifanyi vizuri,”alisema.
Alisema umefika wakati Simba lazima waondokane na hali hiyo na katka hilo, amesema hakuna haja ya kuoneana haya wala kuogopana.
“Nafikiri watu wengi wanasema kama mimi naweza kuburuzwa, mimi siburuziki, mimi nasema ukweli, kama tatizo lipo litatuliwe,”alisema.
Mama huyo ameshauri matatizo ndani ya Simba yaanze kutatuliwa kuanzia ndani ya uongozi, akiwashauri wakae chini na kutafuta suluhisho la muda mrefu.
“Siyo mambo ya kuzima zima moto, au mambo ya kuweka weka viraka, kama hili tatizo la kocha, ni la kukaa tu na kocha mwenyewe na kulitatua. Lakini mtu wao wenyewe wamemuita, amefika hapa wanamkwepa, akianza kusema sema maneno, kosa litakuwa la nani, kosa litakuwa la uongozi dhahiri.
Mimi nasema, nitalitatua hili tatizo, nitampa kocha fedha zake kwa sababu ni haki yake. Mtu katoka kwao kule, amekwishawafanyieni kazi, mpeni haki yake, ya nini mnamzungusha? “alihoji Malkia wa Nyuki.
Aidha, Malkia wa Nyuki amekana dhana kwamba yeye anaburuzwa ndani ya Simba, akisema; “Kwa hiyo mimi nasema, nawaambia watu wa Simba, hamna mtu anayeniburuza hapa, wala siogopi mtu, kitu kinachotakiwa tuanze kujisafisha,”alisema.
Amelaani kitendo anachofanyiwa Milovan, akisema inawezekana klabu hiyo ikamuhitaji tena baadaye, hivyo halitakuwa jambo zuri kuharibu uhusiano naye.
“Kwa hiyo ninamuomba msamaha kocha kwa matatizo yote, amenipa data zake za benki, nasafiri leo, nataka acheki akaunti yake Jumatano atapata fedha zake,” alisema.
Pamoja na hayo, Mama huyo amesema hakuridhishwa na kiwango cha timu, ambayo sasa iko chini ya kocha Mfaransa, Patrikc Liewig katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Recreativo de Libolo ya Angola, siku ambayo Wekundu hao wa Msimbazi walilala 1-0 nyumbani.
Simba ambayo ina makocha wasaidizi watatu, wazalendo Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ na James Kisana na Mganda, Moses Basena sasa inatakiwa kushinda 2-0 ugenini wiki ijayo ili kusonga mbele kwenye michuano hiyo.
Milovan alitimuliwa Simba SC baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Novemba mwaka jana timu hiyo ikishika nafasi ya tatu nyuma ya Yanga, inayoongoza hadi sasa na Azam inayoshika nafasi ya pili hadi ya sasa.
Malkia wa Nyuki kulia akimsikiliza Milovan |
Milovan kushoto akimsikiliza Malkai wa Nyuki |