Na Bin Zubeiry |
Yanga ilishinda 1-0 kwa tabu. Huo ndiyo usahihi. Ilionekana dhahiri timu zote zilijiandaa kwa ajili ya kukabiliana. Kila timu ilifanyia kazi ubora na udhaifu wa mpinzani wake.
Makocha wote walikuwa wana hofu ya kupoteza mchezo, wakapanga vikosi kwa umakini na kutumia mifumo madhubuti.
Viungo walikuwa wengi sana uwanjani jana, kwa mfano upande wa Azam, kiungo mmoja mwenye sifa ya ukabaji wa hali ya juu, Ibrahim Mwaipopo alicheza. Kiungo mwingine mkabaji mzuri, Kipre Balou jana alichezeshwa beki ya kulia.
Bado kukawa na viungo wengine wakiongozwa na Salum Abubakar ‘Sure Boy’, wakati mshambuliaji kwa maana ya mshambuliaji, alikuwa mmoja tu, John Bocco ‘Adebayor’.
Kipre Tchetche tunamuita mshambuliaji, lakini anatumika kama kiungo wa pembeni, isipokuwa jamaa anashambulia sana.
Ukienda Yanga, walikuwa wana safu imara sana ya kiungo, ikiundwa na Frank Domayo, Athumani Iddi ‘Chuji’ na Haruna Niyonzima.
Mabeki wa Azam walimzibia kabisa njia kiungo wa pembeni matata wa Yanga, Simon Msuva na mshambuliaji Jerry Tegete pamoja na kupata nafasi tatu nzuri akashindwa kuzitumia, lakini pia aliwekewa ulinzi mkali.
Kupoteza nafasi kwa Jerry, bila shaka ni kwa sababu zilikuja katika wakati ambao hakutarajia, kutokana na jinsi alivyodhibitiwa.
Alifanikiwa kutumbukiza mpira mmoja, nyavuni lakini wakati akiwa tayari amekwishaotea na refa Hashim Abdallah alikuwa makini katika hilo.
Yanga walicheza kwa nidhamu ya hali ya juu na woga ndani yake, haswa baada ya kupata bao. Walionekana kutaka pointi tatu zaidi kuliko ushindi mnono. Hii maana yake walijua wanacheza na timu nzuri.
Ukirejea kipindi cha pili mchezo ulivyokuwa, ilionekana kama Yanga walizidiwa, lakini hilo lilitokana na mchecheto na wachezaji wao, kuhofia kufungwa na kuelekeza akili zao katika kujihami zaidi.
Walitumia mbinu nyingi sana, kubwa zaidi kupoteza muda kwa kujiangusha angusha, kuchelewa kuanzisha mchezo na kadhalika.
Kuna wakati kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ aliingiza mpira wa pili uwanjani, wakati Didier Kavumbangu ameanguka na akapambana na Seif Abdallah kugombea mpira huo, yote hiyo kuuchelewesha mchezo.
Karibu kila mpira wa juu aliodaka Barthez, alipofika chini hakuinuka kwa madai ameumia na alitibiwa si chini ya mara nne kwa muda usiopungua dakika tatu katika kila tukio, maana yake kipa huyo alipoteza wastani wa dakika 12, peke yake.
Ukiurejea kwa makini mchezo wa jana, dakika zisizopungua 20 zilipotezwa, kwa sababu hata kipa wa Azam, Mwadini Ally kuna wakati alilala. Wachezaji walianguka sana, haswa wa Yanga.
Lakini refa alichezesha kwa haki, isipokuwa wachezaji wa Yanga walimzidi ujanja. Kuna wakati mchezaji wa Yanga aliunawa mpira katika eneo la hatari, lakini kwa kuwa alikuwa amempa mgongo refa, hakuona.
Kweli zilikutana timu ambazo zinapigania ubingwa na kama ambavyo alisema kocha wa Yanga, mechi ya jana kwao ilikuwa kama fainali, kweli walifanikiwa kushinda fainali.