Rais wa ZFA, Amani Makungu |
Na Ally Mohamed, Zanzibar
KMKM
imeanza vyema mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Zanzibar, maarufu kama Zanzibar
Grand Malt Premier League, baada ya kuichapa Mafunzo mabao 2-1 kwenye Uwanja wa
Mao Tse Tung, Kisiwani Unguja jana.
KMKM
ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa mshambuliaji wao tegemeo Maulid
Ibrahim katika dakika ya 35 ya kipindi cha kwanza, mpaka mapumziko matokeo
yalikuwa yanasomeka 1-0.
Kipindi
cha pili katika mchezo huo kiliingia dosari baada ya mchezaji wa KMKM Faki
Mwalim kutolewa nje kwa kadi nyekundu kufuatia mchezo mbaya.
Mafunzo
walifanikiwa kusawazisha katika dakika ya 79 kupitia kwa Ame Khamis, hata hivyo
bao hilo halikudumu kwani licha ya KMKM kucheza pungufu mchezaji mmoja
walifanikiwa kupata bao la ushindi katika dakika ya 82 kupitia kwa Jaku Joma.
Kwa
matokeo hayo KMKM wanaendelea kuongoza msimamo wa ligi hiyo baada ya kufikisha
pointi 26 wakifuatiwa na Mafunzo yenye pointi 22.
Katika
mchezo mwingine, uliofanyika kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba, mabingwa watetezi
wa ligi hiyo, Super Falcon wamefanikiwa kuanza vyema mzunguko wa pili baada ya
leo kuchomoza na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Chipukizi ya Chake Chake.
Bao
pekee la ushindi kwa Super Falcon lilifungwa katika dakika na Omar Mohammed
katika dakika ya 69.
Ligi
hiyo inatarajia kuendelea tena kesho katika viwanja viwili tofauti katika
visiwa vya Unguja na Pemba. Kisiwani Pemba katika Uwanja wa Gombani kutakuwa na
pambano kati ya Duma timu inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Uchumi Kisiwani
Pemba, ikionyeshana kazi na Jamhuri ambao tarehe 16 ya mwezi huu watakuwa na
mechi ya Kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika watakapoikaribisha St.
George kutoka Ethiopia kabla ya kurejeana wiki mbili baadae, itakumbukwa kuwa
Jamhuri ambao ni washindi wa pili wa ligi iliyopita walitakiwa kuiwakilisha
Zanzibar katika kombe la Shirikisho lakini kutokana na Mabingwa wa Soka
Zanzibar kuamua kujitoa katika michuanop hiyo kutokana na ukata Jamhuri
wamechukua nafasi hiyo huku Zanzibar ambao ni mwanachama mshiriki wa CAF wakiwa
hawana uwakilishi katika michuano ya kombe la Shirikisho inayoandaliwa na CAF.
Kwa
upande wa Kisiwa cha Unguja hapo kesho kutakuwa na mchezo mmoja katika Uwanja
wa Amaan, ukiwakutanisha Bandari na Malindi.