Kiiza akitoka eneo la lango la Mtibwa baada ya kufunga bao la kusawazisha, kulia Tegete akimpongeza |
Na Mahmoud Zubeiry
YANGA
SC leo imepunguzwa kasi, baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na
Mtibwa Sugar ya Morogoro katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara
uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni hii.
Hadi
mapumziko, Mtibwa walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na kiungo wa
zamani wa Simba SC, Shaaban Kisiga ‘Malone’ dakika ya 44.
Kisiga
aliyewika pia SC Villa ya Uganda na Azam FC ya Dar es Salaam alifunga bao hilo
akiunganisha kwa kichwa kona maridadi ya beki Issa Rashid ‘Baba Ubaya’.
Pamoja
na kufungwa, Yanga ndio waliotawala zaidi kipindi cha kwanza na walikosa mabao
matatu ya wazi, mawili kupitia kwa Didier Kavumbangu na moja Jerry Tegete.
Kwa
ujumla umaliziaji mbovu ndio uliowagharimu Yanga kutoka uwanjani baada ya
dakika 45 za kwanza wakiwa hawajapata bao.
Kipindi
cha pili, Yanga walipigana haswa kusaka mabao, lakini Mtibwa walikuwa imara
hiio leo.
Kipa
Hussein Sharrif ‘Cassillas’ alizuia michomo mingi ya washambuliaji wa Yanga
ambao hakika siku ya leo bahati haikuwa yao.
Alikuwa
ni mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Hamisi Kiiza ‘Diego’ aliyeingia kipindi
cha pili kuchukua nafasi ya Didier Kabumbangu aliyeinusuru Yanga kuzama katika
mchezo wa leo baada ya kufunga bao la kusawazisha dakika ya 86, akiunganisha
pasi nzuri ya Said Bahanuzi aliyetokea benchi pia kuchukua nafasi ya Frank Domayo.
Baada
ya bao hilo, Yanga waliongeza kasi kusaka bao la ushindi, hata hivyo Jerry
Tegete alipoteza nafasi nzuri ya mwisho baada ya kupewa pasi nzuri na Simon Msuva,
lakini akashindwa kuumiliki vyema mpira.
Matokeo
hayo yanaifanya Yanga itimize pointi 33 baada ya kucheza mechi 14 na inaendelea
kuongoza Ligi Kuu, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 32, zote zimecheza mechi 14.
Katika
mchezo wa leo, kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu
Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi
‘Chuji’/Nurdin Bakari, Simon Msuva, Frank Domayo/Said Bahanuzi, Didier
Kavumbangu/Hamisi Kiiza, Jerry Tegete na Haruna Niyonzima.
Mtibwa
Sugar; Hussein Sharrif ‘Casillas’, Said Mkopi, Issa Rashid, Rajab Mohamed,
Salum Swedi, Shaaban Nditi, Vincent Barnabas, Rashid Gumbo, Hussein Javu,
Shaaban Kisiga ‘Malone’ na Ally Mohamed ‘Gaucho’.